Kila tone la maji ni muhimu  kwa dunia hii-WMO

23 Machi 2020

Mafuriko, mvua za kupindukia, ukame na kuyeyuka kwa barafu ni ishara kubwa ya mabadiliko ya tabianchi yanayohusisha maji limesema shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO.

Katika ujumbe wake maalum kuhusu siku ya utabiri wa hali ya hewa duniani hii leo shirika hilo linasisitiza ujumbe wa siku ya maji duniani kwa kujikita na uhusiano uliopo baina ya mabadiliko ya tabianchi na maji na kutoa wito wa kuhakikisha kuna takwimu bora zinazohusiana na masuala ya maji.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Msataifa Antonio Guterres akiongeza sauti yake katika ujumbe kuhusu siku hii amesema “Mabadiliko ya tabianchi na maji havitengamani. Vyote ni kitovu cha malengo ya kimataifa ya maendeleo endelevu, mabadiliko ya tabianchi na upunguzaji wa hatari ya majanga.”

Hivyo amesisitiza kwamba “Maji ni moja ya bidhaa ya thamani kubwa sana katika karne ya 21, na huduma za kitaifa za utabiri wa hali ya hewa na upatikanaji wa maji zitakuwa kiungo muhimu cha juhudi za kuhesabu kila tone la maji kwa sababu kila tone ni muhimu.”

 Hatuwezi kudhibiti tusichoweza kukipima: takwimu ni muhimu

Kwa mujibu wa Guterres ongezeko la hali isiyotabirika, mabadiliko ya mwenendo wa hali ya hewa huenda vikaongeza upungufu na shinikizo kubwa katika suala la maji  ambalo linaweza kuathiri malengo ya maendeleo endelevu na usalama.

Katibu Mkuu ameongeza kwamba athari za kutotabirika kwa hali ya hewa zilianishwa kwa kina katika ripoti ya WMO kuhusu hali ya hewa duniani na taarifa ya kwa mwaka 2019 iliyotolewa Machi 10 mwaka huu.

Utafiti umeonyesha kuwa mabadiliko ya tabianchi ynaleta athari katika nyanja zote za mazingira pamoja na katika afya na ustawi wa watu wote duniani.

Mwaka 2019 matukio makubwa na mabaya ya hali ya hewa ambayo si ya kawaida yalikumba sehemu nyingo duniani.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR liliwasaidia maelfu ya watu waliokumbwa na kuathirika na janga la monsoon katika kambi ya wakimbizi wa Rohingya .

Pia ilijumuisha mvua kubwa za monsoon na mafuriko yaliyokatili Maisha ya watu India, kuwa mwaka wenue ukame mkali kuwahi kushuhudiwa Australia na athari kubwa zilizosababishwa na kimbunga Idai nchini Msumbiji na pwani ya Mashariki mwa Afrika.

Hii ndio sababu WMO inataka utabiri na kukusanywa kwa takwimu za masuala ya maji, ufuatiliaji wake na udhibiti wa usambazaji wa bidhaa hiyo muhimu. WMO inasema “hii itasaidia kukabiliana na tatizo la Maji mengi kupita kiasi, machache kuliko inavyotarajiwa na uchafuzi wa maji.”

Shirika hilo limesisitiza kwamba takimu bora zitasaidia katika mipango ya miradi ya maji kama mitambo ya umeme ya uchimbaji wa maji, uboreshaji wa uelewa wa athari za udhibiti wa rasilimali ya maji katika mazingira, uchumi na jamii na pia zinaweza kusaidia kuwalinda vyema watu , mali na mifumo ya maisha dhidi ya majanga yatokanayo na maji hasa mafuriko, ukame na uchafuzi.

Ushirikiano baina ya hali ya hewa na huduma za maji

Kwa sababu ya uwezekano kwamba mustakbali wa maji utahitaji maamuzi magumu hasa linapokuja suala la kugawanya rasilimali WMO inatoa wito wa kuwepo ushirikiano wa karibu baina ya suala la hali ya hewa na huduma za maji.

Akisisitiza hilo mkurugenzi mkuu wa WMO Petteri Taalas amesema “Uwezo kwa ajili ya utabiri , ufuatiliaji na udhibiti wa maji hivi sasa umegawanyika na hautoshelezi. Inatia wasiwasi kuona kwamba lengo la maendeleo endelevu namba 6 (SDG-6) ambalo linajikita na maji safi na usafi hivi sasa haliendi kwenye mstari unaotakiwa.”

Ameongeza kuwa “Dunia inahitaji kuonyesha mshikamano kama ule wa hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kupunguza gesi chafuzi ya hewa ukaa wakati huu wa kudhibiti mlipuko wa janga la COVID 19.”

WMO imesema imedhamiria kufanyakazi kwa karibu na Un water na wadau wengine muhimu wa Umoja wa Mataifa katika uboreshaji wa uetekelezaji na uchapuzaji wa mchakato wa utimizaji wa SDG-6.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter