Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya kufuta maadhimisho sababu ya COVID-19 mabomu ya kutegwa ardhini bado tishio:UN

Mabomu yakiandaliwa tayari kwa ajili ya kuteketezwa
UNMAS
Mabomu yakiandaliwa tayari kwa ajili ya kuteketezwa

Licha ya kufuta maadhimisho sababu ya COVID-19 mabomu ya kutegwa ardhini bado tishio:UN

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umesema pamoja na hatua kubwa zilizopatikana katika kukabiliana na mabomu ya kutegwa ardhibni kote duniani , mabomu hayo bado ni tishio kubwa . 

Hayo yamo katika ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wa kuelekea maadhimisho ya siku ya kimataifa ya uelimishaji na msaada dhidi ya mabomu ya kutegwa ardhini itakayokuwa kesho Jumamosi.
 
Katika ujumbe huo Guterres amesema miongo iliyopita mamilioni ya mabomu ya kutegwa ardhini yalizikwa katika nchi kote duniani. Kuanzia Cambodia hadi Msumbiji, nchini angola na Afghanistan maelfu ya maisha ya watu yalipotea na ya wengine kubadilika daima kwa sababu ya hatua moja ya bahati mbaya.

Ameongeza kuwa kilio cha asasi za kiraia mwanzoni mwa miaka ya 1990 kilisukuma mfumo wa kimataifa kuchukua msimamo dhidi ya matumizi ya mabomu ya kutegwa ardhini, uliopelekea kuanzishwa mwaka 1997 kwa mkataba wa kupiga marufuku matumizi ya mabomu hayo na mikakati mingine muhimu.

Na kwamba, “leo hii nchi nyingi zimejitangazia kuwa huru bila mabomu hayo na zingine ziko mbioni. Kwa sasa dunia inakabiliwa na jinamizi kubwa la kiafya. Hatari zinazotokana na virusi vya Corona, COVID-19 zinalazimisha kila nchi na kila mtu kuchukua hatua ambazo zingeonekana haziwezekani wiki kadhaa zilizopita.”
 
Hivyo amesema ni kwa sababu hii kwamba maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya kimataifa ya uelimishaji kuhusu mabomu ya kutegwa ardhini yameondolewa.

Mashindano ya mpira wa miguu yaliyotarajiwa kufanyika kwenye ardhi iliyosafishwa na kuondolewa mabomu yote ya ardhini yamefutwa, hafla ambazo zinalenga kuleta pamoja jamii ya wanaochukua hatua dhidi ya mabomu hayo sasa itafanyika kwa njia ya mtandao endapo itawezekana,.

“Walakini hata katikati ya janga hili hatuwezi kuiacha siku hii ikapta hivihivi tu, hatuwezi kuruhusu haki za watu wenye ulemavu kutotekelezwa.Mabomu, mabaki ya vifaa vya vita vya mlipuko na vilipuzi vingine vinatishia baadhi ya watu walio katika mazingira magumu kwenye jamii wakiwemo wanawake wanaokwenda masokoni, wakulima wafugaji wa ng’ombe, wahudumu wa kibinadamu wanaojaribu kuwafikia wale walio na uhitaji mkubwa.” Amesema. 

Katibu Mkuu amesema zaidi ya hayo mafanikio ya jumuiya ya kuchukua hatua kupambana na mabomu ya kutegwa ardhini yanaonyesha kwamba, “kwa kufanyakazi pamoja tunaweza kufikia hatua ambayo awali ilionekana haiwezekani, ujembe wa wakati muafaka kwa juhudi zetu leo hii ni kudhibiti maambukizi ya janga la COVID-19.” Kwa mantiki hiyo Katibu Mkuu ametoa wito, “hebu na tukumbuke watu wanaoishi katika kivuli cha vifaa vya mlipuko, kuanzia Syria hadi Mali na kwingineko. Wakati watu wengi kote duniani wanafanyia kazi nyumbani salama bado watasalia kuwa katika hatari. Na wakati dunia itaibuka kutoka kwenye janga hili wataendelea kuhitaji msaada wetu.”

Siku ya kimataifa ya uelimishaji na msaada dhidi ya mabomu ya kutegwa ardhini huadhimishwa kila mwaka Aprili 4