Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi 494 kwenye vituo vya afya yameua wagonjwa na wahudumu wa afya 470 katika kipindi cha miaka minne Syria

Picha ya maktaba ikionesha kiliniki za kuhamahama zilizotolewa na WHO ili kusambaza huduma ya afya kwa watu wanaokimbia vurugu mjini Aleppo Syria
WHO Syria
Picha ya maktaba ikionesha kiliniki za kuhamahama zilizotolewa na WHO ili kusambaza huduma ya afya kwa watu wanaokimbia vurugu mjini Aleppo Syria

Mashambulizi 494 kwenye vituo vya afya yameua wagonjwa na wahudumu wa afya 470 katika kipindi cha miaka minne Syria

Amani na Usalama

Shirika la Afya Ulimwenguni WHO kupitia taarifa yake iliyotolewa mjini Geneva Uswisi, Copenhagen Denmark na Cairo Misri limelaani vikali mashambulizi dhidi ya vituo vya afya, ambavyo vimekuwa ishara ya janga la kibinadamu nchini Syria ambalo mwezi huu wa Machi limeingia katika mwaka wake wa kumi.

Mkurugenzi wa dharura wa WHO kanda ya Mashariki mwa Mediterania Bwana Richard Brennan amesema, “takwimu tunazoweza kuweka wazi hivi sasa kuhusu mashambulio dhidi ya afya nchini Syria ni ushahidi mbaya kwa dharau mbaya dhidi ya sheria za kimataifa za kibinadamu na maisha ya raia na wafanyikazi wa afya.”

Katika migogoro yote ya silaha ulimwenguni kote, Syria kwa miaka mingi imekuwa mfano mbaya zaidi wa vurugu zinazoathiri huduma ya afya. Mashambulizi ya makusudi yanayoelekezwa mahali ambako wagonjwa na waliojeruhiwa wanatibiwa, au kuzuia au kuwakatalia raia kupata huduma za afya, inazuiliwa chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu. Mashambulizi ya kipropaganda katika maeneo ya raia pia yanaweza kusababisha uharibifu wa huduma ya afya na kuahatarisha maisha na ustawi wa wale walioko hatarini zaidi.

“Kinachositikitisha ni kuwa tumefikia mahali ambapo mashambulio dhidi ya afya, jambo ambalo jumuiya ya kimataifa haitakiwi kuvumilia, hivi sasa hyatiliwi maanani, kitu ambacho tumezoea. Na bado yanafanyika.Wiki mbili zilizopita, hospitali mbili katika eneo la Idleb zilishambuliwa, wakajeruhiwa wafanyakazi wanne na kwa muda huduma zikasitishwa.” Amesema Brennan.

Taarifa hiyo ya WHO imeendelea kueleza kuwa jumla ya mashambulizi 494 dhidi ya vituo vya afya yalithibitishwa kati yam waka 2016 na 2019 ambapo asilimia 68 ya matukio hayo sawa na visa 337 yalirekodiwa kaskazini magharibi mwa Syria, miongoni mwa maeneo ambayo ni ya mwisho ambayo hyako chini ya mamlaka za serikali. Takwimu zinaonesha kuwa mashambulizi kwenye vituo vya afya yalifikia kiwango cha juu katika mwaka 2016 na yalikuwa kwa kiwango cha chini mwaka jana 2019, pengine kutokana na kupungua kwa eneo ambako mpingo yanyoendelea yalikuw yakifnyika.

Jumla ya vifo vilivyotokana na mashambulio katika huduma ya afya kati ya mwaka 2016 na 2019 ni 470 ambapo kwa mwaka 2016 vilifikia 241 kwa vifo vilivyothibitika. Idadi ya chini zaidi ni 54 iliyorekodiwa mwaka 2019.

Mbali na vifo vilivyotokea, watu 968 walijeruhiwa na mashambulizi haya nchini Syria tangu mwaka 2016, ambapo wengi wao wamebaki na ulemavu wa kudumu.

Kwa mwaka huu wa 2020 mashambulizi ambayo yamethibitika dhidi ya afya ni 9 ambapo yote yametokea kaskazini magharibi na kusababisha vifo 10 na majeruhi 35.