Raia 49 wauawa ndani ya siku 5 Syria hili linatupa hofu kubwa:UNHCR

7 Februari 2020

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa leo imesema inatiwa wasiwasi mkubwa na ongezeko la kasi la machafuko Kaskazini Magharibi mwa Syria na kudharauliwa kwa ulinzi wa raia.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis msemaji wa ofisi hiyo ya haki za binadamu OHCHR, Marta Hurtado amesema mapigano yanayoendelea maeneo ya Kusini na Mashariki mwa Idlib na Magharibi na Kusini mwa Aleppo nchini humo yanaendelea kukatili maisha na kujeruhi mamia ya raia na pia kuwatawanye wengine kwa maelfu. Na kwamba

(SAUTI YA MARTA HURTADO)

“Katika muda wa siku tano kuanzia Februari 1 hadi 5 tumebaini matukio ambapo takribani raia 49 wakiwemo wanawake 14 na watoto 17 wameuawa na kati ya idadi huyo 7 wameuawa katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali

Ameonmgeza kuwa mwezi uliopita pia ofisi hiyo ya haki za binadamu ilibaini kwamba raia 186 wakiwemo wanawake , wavulana na wasichana waliuawa na miongoni mwao raia 14 waliuawa katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali.

Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu Michelle Bachelet amerejea wito wake wa kuzitaka pande zote katika mzozo ikiwemo serikali ya Syria, Urusi, Uturuki na wadau wengine wa kiserikali ama la kuhakikisha ulinzi wa raia na kuendesha operesheni zao za kijeshi kwa kuzingatia sheria za kimataifa.

(MARTA HORTADO)

Inashangaza kwamba raia wanaendelea kubeba mzigo wa uhasama kati ya pande zote katika mzozo. Inaonekana nguvu za kigeni zinapigania faida za kitaifa na kisiasa, huku zikipuuza kabisa jukumu lao la kulinda raia.”

Ameongeza kuwa raia wanaendelea kuuawa hata wakati wakijaribu kukimbia mapigano ili kuokoa roho zao Febriari 3kuliripotiwa mashambulizi ya anga yaliyofanywa na upande wa serikali ambapo moja ya makombora liliangua kwenye basi lililokuwa likisafiri kuelekea Aleppo vijijini na raia 9 kutoka familia moja waliokuwa wakikimbia machafuko waliuawa.

Na tangu tarehe mosi hadi 5 mwezi huu mashambulizi ya anga yaliyofanya na makundi yenye silaha ambayo si ya serikali makombora yalianguka katika makazi ya watu na kwenye vituo vya elimu mjini Aleppo, ambapo raia watano akiwemo mwanamke mmoja na watoto wake wawili waliuawa kwenye eneo la al-Hamdaniya. Kombora pia lilianguka kwenye chuo kikuu cha Aleppo na kujeruhi mwanafunzi mmoja.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud