Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19: Mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu waahirishwa

Ukumbi wa Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa ambamo kwalo wataalamu wa haki za binadamu huchangia hoja kuhusu haki za binadamu
UN Photo - Jean-Marc Ferre
Ukumbi wa Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa ambamo kwalo wataalamu wa haki za binadamu huchangia hoja kuhusu haki za binadamu

COVID-19: Mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu waahirishwa

Afya

Kuendelea kusambaa kwa virusi vya Corona, COVID-19, kumesababisha vyombo vya Umoja wa Mataifa kuahirisha mikutano yake na chombo cha hivi karibuni kabisa kuchukua hatua ni Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ambalo limetangaza hii leo kusitisha mkutano wake wa mwaka kuanzia kesho Ijumaa.

Uamuzi huo umetangazwa na Rais wa Baraza hilo Balozi Elisabeth Tichy-Fisselberger kutoka Austria.

"Baraza limechukua uamuzi huu kusitisha mkutano wake wa 43 wa mwaka kutokana na virusi vya Corona. Kwa wiki nzima ya kwanza ya mkutano huu, Baraza limekuwa likichukua hatua makini kama vile kuhamisha mkutano wake kutoka chumba namba XX hadi ukumbi mkubwa wa Baraza, kupunguza idadi ya viti vya wajumbe na wawakilishi wa mashirika ya kiraia, " amesema Rais huyo wa Baraza la Haki za Binadamu hii leo akitangaza uamuzi huo kwa waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi.

Amesema pamoja na hatua hizo za awali, tangazo la jana la WHO ya kwamba COVID-19 ina dalili za kuenea duniani kote na kwamba imesambaa kwa nchi zaidi y a 100 na kupitia mapendekezo ya serikali ya Uswisi, na ofisi ya Umoja wa Mataifa Geneva, UNOG na shaka na shuku miongoni mwa wajumbe tumeona ni vyema kusitisha vikao."

Balozi Tichy-Fisselberger amesema vikao vinaahirishwa kuanzia kesho tarehe13 mwezi Machi baada ya kupitisha mambo mawili ambayo ni , "mosi kuhusu watu waliopaswa kupatiwa majukumu kwa niaba ya Baraza la Haki za Binadamu katika mkutano hu una lingine kuongeza muda wa wale wenye majukumu ambao wanapaswa kuongezewa muda la sivyo muda wao utamalizika,"

Ameongeza kuwa wataendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa virusi vya Corona na watasikiliza kile kisemwacho na WHO na mamlaka za Uswisi, ambao ni wenyeji wao na kwamba, "huduma za usimamizi wa mikutano wamewahakikishia kuwa watatusaidia kuandaa mkutano huo pindi itapokuwa salama kuitisha tena mkutano huo."