Programu ya kupatia wakimbizi wa Syria fedha Uturuki yawa nguzo ya maisha yao

10 Machi 2020

Mzozo wa Syria ukiingia mwaka wa 10, programu ya shirika la mpango  wa chakula duniani, WFP wa kupatia fedha wakimbizi wa Syria umekuwa na mhimili mkubwa wa kuepusha wakimbizi miioni 1.7 wasitumbukie kwenye umaskini.

Vita nchini Syria vimefurusha raia milioni 5.6 nje ya nchi yao na kwa waliokimbilia Uturuki, program hiyo iitwayo mfuko wa dharura wa kujikimu, ESSN na inayofadhiliwa na Muungano wa Ulaya imekuwa ni nguzo ambapo familia zinazopokea msaada zimeweza kukimu mahitaji muhimu ikiwemo chakula.

Kupitia ESSN kila mwanakaya anapatiwa takribani dola 22 kwa mwezi na fedha hizo zinawekwa kwenye kadi ambapo familia inaweza kuzitoa kwenye mashine ya fedha au kulipia mahitaji madukani.

Familia inaweza kutumia kwa manunuzi yoyote lakini utafiti wa WFP umeonesha kuwa wakimbizi hao wanalipia pango, huduma muhimu chakula na matumizi mengine kama asemavyo mmoja wa wanufaika Amira, ambaye alifika Uturuki mwaka 2014 na mumewe ambaye sasa anafanya kazi kwenye duka dogo la samani anasema,“Kadi ya msaada imetusaidia kwa njia nyingi wakati wa majira ya baridi kali, kama vile kupasha joto nyumba, kununua nguo za watoto na hata sisi wenyewe. Imetusaidia kununua nguo wakati wa majira ya joto na hata mboga za majani, chakula, maziwa kwa watoto. Kadi imetusaidia mengi na twatumai maisha yetu yatakuwa bora alimradi itaendelea kuwepo.”

Nils Grede ni afisa wa WFP na anathibitisha umuhimu wa kadi hiyo, “mwezi Mtukufu wa Ramadhani uliopita, nilitembelea kaya ya wakimbizi ya m ane mmoja na bintize watatu. Mama huyo kwa miaka kadhaa mfululizo hakuweza kuandaa futari ya asili kwa binti zake kwa sababu hakuwa na  jiko la kuoka. Mwaka huu angalau mradi  huu umemwezesha kununua jiko hilo na kuandaa mlo kwa wasichana wake.”

ESSN ni mradi mkubwa zaidi wa kibinadamu  unaofadhiliwa na EU ambapo WFP kila mwaka hupokea dola bilioni 1.4 tangu mwaka 2016 kuutekeleza.

Uturuki inaongoza duniani kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya wakimbzi wa Syria ambao ni takribani milioni 3.6.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter