Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ahsante EU kwa msaada wako kwa watu wa Gaza- WFP

Taka zilizorundikana katika eneo la Ash Sheikh Radwan mjini Gaza.
OCHA
Taka zilizorundikana katika eneo la Ash Sheikh Radwan mjini Gaza.

Ahsante EU kwa msaada wako kwa watu wa Gaza- WFP

Msaada wa Kibinadamu

Muungano wa Ulaya EU umelipatia shirika la mpango wa chakula duniani, WFP zaidi ya dola milioni 3 kwa ajili ya kusaidia kununua chakula cha wapalestina walioko ukanda wa Gaza  huko Mashariki ya Kati.

Taarifa ya WFP iliyotolewa leo mjini Yerusalem inasema fedha hizo zitawezesha  watu maskini takriban 210,000 kununua  chakula wanachotaka kwa kipindi cha mwezi mmoja na nusu, hatua ambayo imekaribishwa na WFP.

Kila familia itapatiwa vocha ya dola 10 kila mwezi na watatumia kununua chakula kutoka maduka tofauti wakati huu ambapo njia za kiuchumi na kijamii za kuwezesha mtu kujipatia kipato Gaza zimesambaratishwa.

Nyumba ya familia ya Palestina katika ukanda wa Gaza ilibomolewa na watawala wa Israel
Photo/UNRWA
Nyumba ya familia ya Palestina katika ukanda wa Gaza ilibomolewa na watawala wa Israel

 

Mwakilishi wa WFP na Mkurugenzi wa shirika hilo huko Palestina Stephen Kearney, amesema kuwa ushirika wao wa muda mrefu na EU unawezesha maskini kumudu maisha  wakati  huu ambapo hali ya uchumi Gaza imedidimia.

Amesema msaada wa chakula kwa WFP pamoja na msaada mwingine wowote ule vinahitajika sasa katika wakati huu mgumu ili kuepuka mgogoro wa kibinadamu.

Tangu mwezi januari mwaka huu WFP imekuwa ikitoa msaada kwa watu maskini 245,000 kupitia mgao wa chakula ama vocha za elektroniki.