Hakuna kinachohalalisha wanawake kuendelea kutengwa-Guterres

6 Machi 2020

Katika kuelekea siku ya wanawake duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Machi 8, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataia amesema kubadilisha uwiano wa mamlaka ni muhimu, sio tu kama suala la haki za binadamu, bali pia kwa ajili ya maendeleo ya kibinafsi, afya na ustawi. 

Antonio Guterres ameyasema hayo leo katika maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani. Siku hiyo kimataifa itaadhimishwa Jumapili. Guterres amesema hakuna kinachohalalisha wanawake kuendelea kutengwa na hivyo,“Ni muhimu kutatua baadhi ya changamoto kubwa na zisizoweza kuepukika za zama zetu. Kutoka kuwakejeli wanawake kuwa ni watu mapepe au walojawa na hisia, hadi kwa maamuzi ya kawaida ya wanawake kulingana na sura zao; kutoka kwenye imani na miiko ambayo inayozunguka kazi za asili za miili ya wanawake, hadi kuangazia na kuwalaumu waathirika,na ufisadi uko kila mahali.”

Katibu mkuu amesisitiza kwamba usawa wa kijinsia utabadilisha maeneo matano muhimu ambayoni mosi,“Utatuzi wa migogoro- Kuhusisha viongozi wa wanawake na watoa maamuzi katika michakato ya upatanishi na amani huchangia amani ya kudumu na endelevu. Pili Mgogoro wa mabadiliko ya tabianchi-Usawa wa kijinsia, ikiwemo wanaume kuongeza juhudi na kuchukua jukumu, ni muhimu ikiwa tunataka kuishinda dharura ya mabadiliko ya tabianchi. Tatu Kujenga uchumi jumuishi- Haki sawa za kiuchumi za wanawake na fursa ni muhimu ulimwenguni kote ikiwa tunataka kuunda utandawazi mzuri ambao unafanya kazi kwa wote.”

Mengine ni nne Kuziba pengo la kidijitali- akisema Hadi pale wanawake watakapokuwa na jukumu sawa katika kubuni teknolojia za kidijitali, ndipo maendeleo ya haki za wanawake yaweza kugeuzwa.

Hivyo amesema ukosefu wa utofauti hautakuza tu usawa wa kijinsia, utaweka ukomo wa uvumbuzi na wigo wa teknolojia mpya, na kuvifanya kutotumika vyema kwa kila mtu.

Na tano, ni Uwakilishi bora wa kisiasa- akisema hii ni hesabu rahisi. Ushiriki wa wanawake unaboresha taasisi.  Karne ya 21 lazima iwe karne ya usawa wa wanawake. Ametoa wito kwa kila mtu “Hebu sote tutimize wajibu wetu katika kutimiza hilo.”

Naye mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake UN Women Phumzile Mlambo-Ngucka katika ujumbe wake kuhusu siku hii akisistiza umuhimu wa usawa wa kijinsia  amesema, Mwaka 2020 ni mwaka wa usawa wa kijinsia, na faida za usawa wa kijinsia sio tu kwa ajili ya wanawake na wasichana, bali  kwa kila mtu maisha yake yatabadilika na dunia yenye usawa ambayo haitomuacha yeyote nyuma. Ni mwaka ambao tunauita kizazi cha usawa. Kwa uongozi wa jumuiya za kijamii tunahamasisha kufikia haki za wanawake na kuadhimisha miaka 25 ya utekelezaji wa jukwaa la Beijing la kuchukua hatua.”

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter