Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tukikumbatia yaliyopita katika usawa wa kijinsia hatuwezi kuganga yajayo katika janga la COVID-19:Guterres

Wanawake mafundi wanaofanyakazi katika kituo cha kuhamisha teknolojia cha mRNA nchini Afrika Kusini
MPP/WHO/Rodger Bosch
Wanawake mafundi wanaofanyakazi katika kituo cha kuhamisha teknolojia cha mRNA nchini Afrika Kusini

Tukikumbatia yaliyopita katika usawa wa kijinsia hatuwezi kuganga yajayo katika janga la COVID-19:Guterres

Wanawake

Ikiwa kesho ni siku ya wanawake duniani Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesisitiza kwamba dunia haiwezi kujikwamua kutoka katika janga la COVID-19 kwa kurejesha saa nyuma katika suala la usawa wa kijinsia. 

Kupitia ujumbe wake wa siku hii Guterres ameainisha mchango mkubwa uliofanywa na wanawake katika jitihada za kutokomeza janga la COVID-19, na kupongeza mawazo yao, ubunifu wao na harakati zao ambazo zinaibadili dunia na kuifanya kuwa bora huku akikaribusha hatua ya kuwa na viongozi zaidi wanawake kote duniani katikia nyanja mbalimbali.

 

Hata hivyo, kama mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alivyoeleza, “mara kwa mara wanawake na wasichana wamebeba mzigo mkubwa wa athari za virusi vinavyosambaa duniani kote, ambazo ni pamoja na wasichana na wanawake kufungiwa shule na maeneo ya kazi, na kusababisha kuongezeka kwa umaskini na unyanyasaji, na kushuhudiwa kwa wanawake wengi kufanya idadi kubwa ya kazi zisizo na malipo duniani lakini za matunzo na huduma muhimu.”

 

Ili kurekebisha hali hiyo, Bwana. Guterres ametoa wito wa kuhakikisha “Elimu bora kwa kila msichana, uwekezaji mkubwa katika mafunzo ya wanawake na kazi zenye staha, hatua madhubuti za kukomesha unyanyasaji wa kijinsia, na huduma za afya kwa wote.”

 

Hatua nyingine zilizopendekezwa na mkuu wa Umoja wa Mataifa ni “pamoja na mgawo wa fursa za kijinsia, ambao unaweza kuufanya ulimwengu kufaidika na viongozi zaidi wanawake.”

 

Wanawake wanachimba mabwawa ya katikati ya mwezi ili kuokoa maji nchini Niger.
©FAO/Giulio Napolitano
Wanawake wanachimba mabwawa ya katikati ya mwezi ili kuokoa maji nchini Niger.

Wanawake na hatua za mabadiliko ya tabianchi

 

 

Kauli mbiu ya siku ya kimataifa ya wanawake mwaka huu ni “usawa wa kijinsia leo kwa ajili ya maendeleo endelevu kesho”, ikisisitiza ukweli kwamba wanawake wanabeba mzigo mkubwa wa athari za janga la mabadiliko ya tabianchi, na kwamba wanahitaji kuwa kitovu cha suluhu za kuwa na sayari endelevu. .

 

Muungano wa kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na haki “The Action Coalition for Feminist Action for Climate Justice”, unasaidia kuhakikisha kuwa hili linafanyika.

 

Muungano huo, unaoleta pamoja serikali, makampuni ya sekta binafsi, mfumo wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia, na ni sehemu ya harakati za kuleta pamoja hatua za kimataifa na uwekezaji, kwa kuzingatia ufadhili wa suluhisho za mabadiliko ya tabianchi zinazozingatia usawa wa kijinsia.

 

Suluhu hizo ni pamoja na kuongeza uongozi wa wanawake katika uchumi unaozingatia mazingira, kujenga uwezo wa wanawake na wasichana kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na majanga, na kuongeza matumizi ya takwimu za usawa wa kijinsia na mabadiliko ya tabianchi.