Tuzibe pengo la teknolojia linaloengua wanawake kwenye maendeleo- UN

Mkunga akipata mafunzo ya mtandaoni katika kambi ya wakimbizi wa ndani mjini Juba, Sudan Kusini
UNMISS/JC McIlwaine for UN Women
Mkunga akipata mafunzo ya mtandaoni katika kambi ya wakimbizi wa ndani mjini Juba, Sudan Kusini

Tuzibe pengo la teknolojia linaloengua wanawake kwenye maendeleo- UN

Wanawake

Hii leo ni siku ya kimataifa ya wanawake duniani ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake amesema ni lazima kuziba pengo la mgawanyiko wa matumizi ya teknolojia kati ya wanawake na wanaume kwa kuwa katika Nyanja hiyo hivi sasa wanawake ni chini ya theluthi moja ya nguvu kazi katika ajira za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati. 

Guterres ametoa kauli hiyo kwa kuzingatia kuwa ujumbe wa mwaka huu unasisitiza matumizi ya teknolojia na ubunifu kama njia ya kusongesha haki na kumkwamua mwanamke. 

“Teknolojia inawea kufungua njia za kupata elimu na fursa kwa wanawake na wasichana. Lakini vile vile inaweza kutumiwa kupazia ukatili na chuki,” amesema Katibu Mkuu na kwamba pindi wanawake wanapokuwa wachache zaidi kwenye teknolojia mpya, ubaguzi unaweza kuanza ‘kupikwa’ tangu mwanzoni mwa ubunifu. 

Ndio maana amesema pengo la kidijitali lazima lizibwe kwa kuongeza uwepo wa wanawake na wasichana kwenye sayansi na teknolojia.  

Siku ya wanawake ni siku ya kufurahia mafanikio 

Siku ya wanawake duniani ni siku ya kufurahia mafaniko ya wanawake na wasichana katika maeneo na nyanja mbali mbali duniani. 

Hata hivyo amesema inatambuliwa kuwa kundi hilo linakabiliwa na vikwazo kuanzia ukosefu wa haki wa kimfumo, kuenguliwa, ukatili hadi majanga yanayoshamiri kila uchao na kuwaathiri wao kwanza bila kusahau yale yanayowanyima haki na miili na maisha yao. 

Ukatili wa kijinsia unamuumiza kila mtu – wanawake, wasichana, wavulana na wanaume, amesema Guterres akisema sasa siku ya leo ni siku ya kutoa wito wa hatua. 

Hatua za kushikamana na wanawake ambao wanataka haki zao za. Hatua za kuimarisha ulinzi dhidi ya ukatili wa kingono na unyanyasaji. Hatua ya kuchagiza ushiriki wa wanawake kwenye uongozi. 

Kuwekeza kwa wanawake kunainua jamii nzima 

“Katika muongo uliopita, kuenguliwa kwa wanawake kwenye dunia ya kidijitali kumepoteza takribani dola trilioni 1 za pato la ndani la taifa kwenye nchi za kipato cha chini na cha kati,” amesema Guterres akiongeza kuwa hasara hiyo inaweza kuongezeka na kufikia dola trilioni 1.5 mwaka 2025 iwapo hatua hazitachukuliwa. 

Katibu Mkuu amesema ni vema ikumbukwe kuwa kuwekeza kwa wanawake kunainua watu, jamii na nchi, kwa hivyo basi “hebu tuwe na ushirikiano mtambuka- serikali, sekta binafsi na mashirika ya kiraia ili kujenga dunia jumuishi zaidi, yenye haki na ustawi ambamo kwamo wanawake, wasichana, wanaume na wavulana kila mahali.”