Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunafanya kila tuwezalo kuwasaidia waathirika wa vita Idlib:WFP

Vipimo vya joto ni nyuzi joto chini ya selsiasi 10 nchini Syria
WFP/Fadi Halabi
Vipimo vya joto ni nyuzi joto chini ya selsiasi 10 nchini Syria

Tunafanya kila tuwezalo kuwasaidia waathirika wa vita Idlib:WFP

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula  duniani WFP limesema linafanya kila liwezalo kuwasaidia watu zaidi ya milioni moja waliokwama katika eneo la Arihah jimboni Idlib nchini Syria kwa mahitaji ya msingi ya kibinadamu hasa chakula. 

Mjini Arihah ni dhahiri kwamba vita vimesambaratisha mji huu na kilichosalia ni magofu tu na maelfu ya watu wakiwemo watoto sasa wanaishi katika kambi ya Ma`arrat Misrin iliyoanzishwa Desemba mwaka 2019 baada ya vita na mashambulizi ya makombora kushika kasi Kusini mwa Idlib na kuwafanya mamia kufungasha virago.

Takribani familia 500 zikaishia kambini hapa akiwemo Nisrine Alomar mwenye umri wa miaka 30. Alikuwa mkulima na ametawanywa mara saba katika kipindi cha miaka 9 ya vita vya Syria na mwaka jana makombora yalimlazimisha yeye na watoto wake saba kukimbia eneo la Saraqib , ilibidi wachifiche na kulala chini ya miti hadi walipofanikiwa kuwasili kambini hapa, “Kila wakati mashambulizi ya mabomu yanapotokea tunaogopa sana na watoto wanalia”

Kwa sasa WFP inawapa msaada wa chakula ambacho kipo tayari kuliwa ikiwemo siagi itokanayo na mboga za jamii ya maharage na kunde, kuku wa makopo na mbogamboga, kwa wakimbizi wapya wanaowasili  na mgao wa mwezi mmoja wa unga wa ngano au mikate, mchele, unga wa Bulga, sulari, chumvi, na mafuta ya kupikia. Jopo la wafanyakazi wa WFP limezuru eneo hilo kushughudia operesheni za msaada akiwemo mkurugenzi mtendaji David Beasley, “Katika nchi nzima tunawasaidia takribani watu milioni 4.5 lakini katika eneo hili karibu watu milioni moja. Haijalishi uko Kaskazini au Kusini mwa Idlib tunafanya kila tuwezalo  ili kuwafikia watu wote wenye mahitaji bila kujali wanamsimamo gani wa kisiasa au walipo kijiografia.”

Ameongeza kuwa hiyo ndiyo kazi ya WFP kujaribu kuleta matumaini na uaina fulani ya uhakika wa chakula katika eneo ambalo linahitaji msaada mkubwa.