Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ni mbaya huku watu wakiendelea kutawanywa Syria:UN Ripoti

Watoto wanacheza katika kambi ya watu waliofurushwa kusini mwa Idlib nchini Syria.
UNOCHA
Watoto wanacheza katika kambi ya watu waliofurushwa kusini mwa Idlib nchini Syria.

Hali ni mbaya huku watu wakiendelea kutawanywa Syria:UN Ripoti

Amani na Usalama

Tume ya Umoja wa Mataifa ya uchunguzi kuhusu machafuko yanayoendelea nchini Syria imesema hali ni mbaya na vita nchini humo havina dalili yoyote ya kumalizika, huku ukiukwaji wa haki za binadamu ukiongezeka.

Katika ripoti iliyochapishwa leo na tume hiyo mjini Geneva Uswisi inayo,mulika kuanzia 11 Julai 2019 hadi 10 Januari 2020 tume hiyo imesema karibu miaka 9 tangu kuzuka kwa vita Syria “wanawake, watoto na wanaume wanaendelea kukabiliwa na madhila na uchungu wa hali ya juu.”

Ripoti inasema katika kutangaza vita dhidi ya ugaidi vikosi vinavyounga mkono serikali “vimefanya mashambulizi ya anga na ardhini Kusini mwa Idlib ambayo yameua na kujeruhi idadi kubwa ya raia na kuharibu miundombinu ya raia ikiwemo masoko, makambi kwa ajili ya wakimbizi wa ndani na pia hospitali.”

Imeongeza kuwa mashambulizi hayo yamewaacha raia bila chaguo lolote isipokuwa kufungasha virago na kukimbia. “Asilimia kubwa ya watu 948,000 waliotawanywa Kaskazini Magharibi mwa Syria ni wanawake na watoto, huku maelfu wakipata hifadhi katika maeneo ya wazi katika miezi hii ya msimu wa baridi kali” imesema ripoti hiyo.

Ripoti imesisitiza kwamba mgogoro jimboni Idlib ambako zaidi ya watu milioni 3 wamekwama unageuka kuwa zahma kubwa ya kibinadamu ambapo familia kila wakati zinakimbia na watoto wanakabiliwa na baridi kali hadi kupoteza maisha.

“Makundi yenye silaha yanafanya mashambulizi katika maeneo yanayodhibitiwa na serikali ikiwemo Kusini mwa Aleppo na kusababisha vifo na majeruhi na kuzusha hofu kubwa miongoni mwa raia na kuwafanya maelfu kuondoka.”

Kwa mujibu wa ripoti zaidi ya watu 100,000 walitawanywa ndani ya saa 24 kati ya Oktoba 10 na 11 mwaka jana .

Ripoti imeongeza kuwa katika wilaya ya Afrin kwa mfano wanawake na hasa wale wanaotoka katika makabila na jamii za kidini wameathirika zaidi na vita, “wanawake na wasichana kutoka makabila ya Wakurdi na Yazidi wameshuhudia kukatazwa kutembea na kudhalilishwa wakitoka nje, vitendo hivyo vinakandamiza uwezo wa wanawake kushiriki kikamilifu katika kuchangia kwenye jamii zao na hili ni lazima likome” amesema Kamisha wa tume hiyo Hany Megally.

Ameongeza kuwa pande kinzani katika mzozo zimeendelea kudharau na kutotoa ulinzi ikiwemo kuhakikisha msaada wa kibinadamu unafika bila masharti kwa raia. “Kipaumbele cha haraka ni lazima kiwe kwa raia wote kupata fursa ya chakula, maji na msaada wa madawa wanaouhitaji haraka.

Ripoti hiyo imekamisha kwa kutoa mapendekezo kwa serikali, pande zinazokinzana na kwa jumuiya ya kimataifa kuimarisha ulinzi kwa raia kwa kushiriki kwa nia Njema katika mazungumzo ya kukomesha uhasama na kuruhusu misaada ya kibinadamu bila vikwazo vyovyote.

Ripoti hiyo itawasilishwa tarehe 10 Machi kwenye Baraza la Haki za binadamu.