Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yasitisha mgao wa chakula kwa Wasyria 47,500, kisa usalama

Wakimbizi wa Syria wakiwa mbioni kutafuta makazi
UNICEF/UN0277723/Souleiman
Wakimbizi wa Syria wakiwa mbioni kutafuta makazi

WFP yasitisha mgao wa chakula kwa Wasyria 47,500, kisa usalama

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mastaifa la mpango wa chakula duniani WFP leo limesema limesitisha kwa muda ugawaji wa chakula kwa watu 47,500 nchini Syria kutokana na changamoto za usalama.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswis msemaji wa WFP Herve Verhoosel amesema shirika hilo la WFP na washirika wake linaendelea kusambaza chakula cha moto kilichopikwa na kile ambacho kiko tayari kwa kuliwa kwenye maeneo ambayo hali ya usalama inaruhusu. 

Hata hivyo amesema katika maeneo ambayo miundombinu imeathirika na machafuko wafanyakazi wa wawashirika wametawanywa na miundombinu yao ya kuwawezesha kufikisha misaada ama imeharibiwa au kusambaratishwa kabisa. 

“Kwa mfano ugawaji wa mgao wa chakula Kusini mwa Idlib, Saraqab, Jish Ash Shugur, Maarat An Numan na Kafr Nobol, kwa watu  47, 500  hivi sasa umesitishwa kwa muda tangu siku chache zilizopita kutokana na masuala ya usalama.”

Ndege ya WFP ikisambaza chakula.
Maktaba/UN
Ndege ya WFP ikisambaza chakula.

Amesisitiza kuwa endapo hali itakuwa mbaya zaidi katika eneo la Kaskazini Magharibi , WFP iko tayari kusaidia kwa mikakati ya dharura, mgao wa chakula pamoja na usambazaji wa lishe chakula ambacho kiwemehifadhiwa katika ghala ndani ya jimbo la Idlib Syria na pia kwatika nchi jirani ya Uturuki.

WFP na Umoja wa Mataifa wanaendelea kutoa wito kwa pande zote husika katika mzozo kuwalinda raia kwa gharama yoyote na kuheshimu wajibu wao chini ya sheria za kibinadamu za kimataifa na haki za binadamu.

Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa pande hizo katika mzozo kusitisha uhasama na kuzingatia makubaliano ya amani yaliyotiowa saini kati ya Uturuki na Urusi mwaka 2018.