Skip to main content

“Acheni unyanyapaa dhidi ya wachina na wengine wa Asia Mashariki kisa virusi vya Corona”- Bachelet

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet
UN Photo/Antoine Tardy
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet

“Acheni unyanyapaa dhidi ya wachina na wengine wa Asia Mashariki kisa virusi vya Corona”- Bachelet

Haki za binadamu

Virusi vya Corona vikiendelea kusambamba huku na kule baada  ya kuripotiwa kwa mara  ya kwanza nchini China, hii leo Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Michelle Bachelet amepaza sauti dhidi ya wale wanaotenda vitendo vya chuki na unyanyapaa dhidi ya wachina na watu wa mashariki mwa Asia.

Bi. Bachelet amesema hayo kabla ya kutoa hotuba yake mbele ya Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva, Uswisi hii leo wakati huu ambapo kumeripotiwa taarifa za vitendo vya ukatili na chuki dhidi ya watu wa jamii ya Asia huko barani Ulaya na kwingineko.

“Natoa wito kwa nchi wanachama zichukue hatua zote muhimu kuzuia vitendo hivyo na aina yoyote ile ya ubaguzi,”  amesema Bi. Bachelet.

Kwa mujibu wa shirika la afya  ulimwenguni, WHO, hivi sasa China imesajili wagonjwa 81,000 nchini humo tangu ugonjwa huo ubainike mwishoni mwa mwaka jana.

Mapema leo mamlaka nchini Uswisi, zilithibitisha kisa cha kwanza cha mgonjwa wa virusi vya Corona kwenye mji wa Geneva, ikiwa ni mji wa hivi karibuni zaidi kutangaza kuwa na mgonjwa.

Mapema jana mamlaka za Brazili zilithibitisha kuwepo kwa mgonjwa wa COVID-19, ikiwa ni kisa cha kwanza kwa nchi za Amerika ya Kusini.

Nchini China pekee hadi jana jumatano zaidi ya watu 2700 walishafariki dunia kutokana na ugonjwa huku watu wengine 44 wakifariki dunia katika mataifa 37.

Dalili za ugonjwa wa virusi vya Corona ni mtu kupumua kwa taabu pamoja na homa kali.

“Natuma shukrani zangu za dhati kwa timu za watabibu duniani kote ambao wanakabiliana na virusi vya Corona, virusi ambavyo ni tishio kwa haki ya uhai na afya kwa watu kila mahali,”  amesema Bi. Bachelet.

COVID-19 na haki za binadamu

Akilinganisha ugonjwa huo na jaribio kubwa kwa uwezo wa jamii kukabiliana na majanga, Bachelet amesisitiza kuwa  maadili ya haki za binadamu yanaeleza mwongozo ambao unaweza kuimarisha ufanisi wa hatua zinazochukuliwa.

“Ili kukabiliana vyema na virusi hivyo, hatua zote za kiafya za umma zinapaswa kutekelezwa bila ubaguzi wa aina yoyote ile, na kuwe na uwazi na taarifa zipatiwe watu ili washiriki katika kulinda afya zao,”  amesema Bi. Bachelet

Amekumbusha kuwa karantini zozote ambazo zinazuia uhuru wa mtu kutembea zinapaswa ziendane na hatari iliyopo, kuwe na mudana ziwe salama.

“Haki za wale walio kwenye karantini lazima zilindwe ikiwemo haki ya kupata chakula, maji safi na salama na haki ya kutendewa kiutu na kupata tiba na taarifa na aweze kujieleza,” amesema Bi Bachelet.

Kwa mujibu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO, ugonjwa huo ni hatari zaidi kwa watu wazima na wale wanaougua magonjwa hatari kama vile shinikizo la damu na kisukari.

“Watu wanaoishi kwa pamoja kwenye taasisi ikiwemo wazee na wanaoshikiliwa wanaweza kuwa hatarini zaidi kupata maambukizi,”  amesema kamishna huyo mkuu wa haki za binadamu.

TAGS: OHCHR, COVID-19, Michelle Bachelet, CoronaVirus, Corona