COVID-19 ni jaribio kubwa la uongozi duniani- Bachelet

9 Aprili 2020

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amesema janga la ugonjwa wa virusi vya Corona, au COVID-19 ni jaribio kubwa sana la uongozi hivi sasa.

Akihutubia mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa hii leo katika kikao chake cha kwanza kabisa kufaniyka kwa njia ya video, Bi. Bachelet amesema, "janga hili linahitaji hatua na uamuzi wenye ubunifu kutoka kwa watu wote na kwa ajli ya watu wote. Hii leo tuko mbali kimwili lakini lazima tusimame kwa mshikamano."

Amewaeleza wajumbe kuwa COVID-19 inaleta machungu kila eneo duniani na kutishia haki za binadamu, "kama ambavyo Katibu Mkuu Antonio Guterres ameonya, inatishia siyo tu maendeleo lakini pia ukosefu wa utulivu, ghasia na machafuko."

UN Photo/Jean-Marc Ferré
Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu.

Kamishna Mkuu amesema mikakati muhimu inapaswa kuchukuliwa ili kuimarisha mifumo ya afya na ya kijamii ili kuhakikisha kuwa kuna msaada mkubwa na wa kutosha kwa watakaoathirika na gonjwa hilo akieleza kuwa ni bayana hakuna yeyote anayepaswa kuchwa nyuma katika juhudi za kujinasua.

Mataifa yanajitahidi kulinda haki za binadamu

Bi. Bachelet amesema kuwa nchi zinakabiliwa na changamoto nyingi na nyingine nyingi zinajitahidi kutekeleza ahadi zao za kulinda haki za binadamu wakati huu wa janga la Corona.

Hata hivyo amesema nchi nyingine nazo zinapaswa kushawishiwa kufanya hivyo ili kuhakikisha hatua za kukabili COVID-19 zinakuwa fanisi kwa kila mtu ndani ya nchi yake na duniani kote akiongeza kuwa, "ni dhahiri kuna vipaumbele vya kitaifa lakini hapa ni vyema mataifa yashikamane."

 

COVID-19 imeibua ukosefu wa usawa

Kamishna Mkuu huyo wa haki za binadamu amegusia suala la ukosefu wa usawa lililojitokeza wakati huu wa kukabiliana na janga la Corona akisema kuwa ugonjwa umefichua hali hiyo.

"Katika nchi tajiri nyufa zimefichuka katika upatikanaji wa huduma za afya, ajira na hifadhi za kijamii; maeneo ya makazi. Katika nchi maskini, ambako idadi kubwa ya watu wanategemea kipato cha siku kwa siku, madhara yanaweza kuwa makubwa zaidi," amefafanua Bi. Bachelet.

Ameeleza kuwa suala kwamba tishio la virusi hivi linagusa dunia nzima, hoja nzito ya siku zote ya utatuzi ni ni uwepo wa huduma ya afya kwa wote, kuimarisha mifumo ya huduma za afya kwa kila nchi na hili ni jambo la dharura.

Bi. Bachelet amesema kwamba mikakati thabiti na ya kina ya kiuchumi na kijamii inapaswa kuchukuliwa pia, katika kila nchi ili kupunguza mshindo wa athari za COVID-19 kwa jamii na ili hatimaye kupunguza pengo la ukosefu wa usawa. "Nchi nyingi zinazoendele hazina uwezo wa kuhimili au kupunguza madhara ya kiuchumi na kijamii yatokanayo na COVID-19 na zinaweza pia kuwa waathirika wa mdororo wa kiuchumi kupitia ongezeko la bei za bidhaa na kushuka kwa uwekezaji wa vitegauchumi vya kigeni au hata utumaji wa fedha kutoka nje," amefafanua Kamishna Mkuu.

Hata hivyo amesema hatua zozote za kuhimili mshindo wa COVID-19 zisisigine haki za binadamu, "nasihi serikali zote ziongeze uwezo wa watu kupata taarifa na takwimu sahihi kwani uwazi ndio msingni wa kuokoa maisha katika janga hili la kiafya. Natoa wito pia kukomeshwa kwa ufungaji wa intaneti. Njia pekee ya kukabili COVID-19 ni umma kuwa na imani na serikali yao."

 

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud