Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yataka nchi ziwasilishe taarifa kuhusu virusi vya Corona

Kipima joto kinachotumiwa kupima viwango vya joto vya wageni kwenye lango la kuingilia hoteli moja huko Yangon nchini Myanmar.
UN News/Jing Zhang
Kipima joto kinachotumiwa kupima viwango vya joto vya wageni kwenye lango la kuingilia hoteli moja huko Yangon nchini Myanmar.

WHO yataka nchi ziwasilishe taarifa kuhusu virusi vya Corona

Afya

Shirika la afya  ulimwenguni, WHO limesema kuwa changamoto kubwa hivi sasa katika kudhibiti kuenea kwa virusi vya Corona, ni nchi nyingine zenye wagonjwa hao kutokuwa tayari kuwasilisha taarifa zao kwa shirika hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Gebreyesus amesema hayo leo wakati wa mkutano wake wa kila siku na waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi wenye lengo la kutoa muhtasari wa hali ilivyo kuhusu ugonjwa huo.

Amesema changamoto hiyo inatiwa wasiwasi mkubwa hasa wakati huu ambapo idadi ya wagonjwa wapya nje ya China imekuwa kubwa.

Nje ya China kuna wagonjwa, 2,790 katika mataifa 37, na vifo ni 44. Jana idadi ya visa vipya nje ya China imezidi idadi ya visa vipya China na hii ni mara ya kwanza. WHO haiwezi kutoa mwongozo sahihi wa afya ya umma bila kuwa na data  mahsusi zilizonyumbuliwa,amesema Dkt. Tedros.

Amesema ni kwa mantiki hiyo hivi sasa wanawasiliana moja kwa moja na mawaziri wa afya, “kuna mafanikio kidogo na tunasihi nchi zote ziwasilishe taarifa zao mara moja WHO.”

Dkt. Tedros amekumbusha kuwa “hatukabiliani tu na virusi au kuokoa maisha. Tunapambana pia ili kudhibiti tatizo la kijamii na kiuchumi ambalo linaweza kusababishwa na janga la kiafya.”

Amesema ni kwa kuzingatia hali hiyo, hivi sasa wanashirikiana na Benki ya Dunia na shirika la fedha duniani, IMF kukadiria kile kinachoweza kuwa madhara ya kiuchumi kutokana na virusi vya Corona, COVID-19, na kuandaa mkakati na sera za kuhimili athari hizo.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa WHO amekumbusha kuwa hivi sasa ni wakati wa mshikamano wa dunia- mshikamano wa kisiasa, kiufundi na kifedha.

Hadi saa 12 asubuhi kwa saa za Geneva, China ilikuwa imeripoti jumla ya wagonjwa 78,190 tangu kuanza kwa mlipuko huo na kati yao hao 2718 wamefariki dunia.

Jana kulikuwepo na wagonjwa wapya 10 nchini China kwenye jimbo la Hubei.

Nchi zifanye nini?

WHO inasema kuwa lengo la msingi hivi sasa ni nchi zenye maambukizi kujaribu kudhibiti virusi hivyo na kwamba hata nchi ambazo hazijakuwa na mgonjwa zijiandae kukabiliana na virusi hivyo kwa kuwa na uwezo wa kubaini, kutenga wagonjwa, kufuatilia wale waliokaribiana nao, kupatia huduma wagonjwa, kuzuia milipuko hospitalini na kwenye jamii.

Kwa mantiki hiyo Dkt. Tedros ametaja vipaumbele vitatu vya WHO kwa nchi hizo akisema kuwa ni, “mosi, nchi zote zipatie kipaumbele kulinda wahudumu wa afya, pili, lazima tushirikishe jamii na kulinda wale walio hatarini zaidi hususan wazee na watu wenye magonjwa mengine, tatu lazima tulinde nchi ambazo ziko hatarini zaidi, kwa kuzuia milipuko kwenye nchi zenye uwezo wa kufanya hivyo.