Janga lililosababishwa na binadamu Syria likome sasa- Guterres

21 Februari 2020

“Hakuna suluhu ya kijeshi kwenye mzozo wa Syria,”  amesisitiza tena hii leo Katibu Mkuu wa  Umoja wa Mataifa António Guterres huku akitoa wito kwa kumalizwa kwa janga hilo lililosababishwa na binadamu na kuleta machungu ya muda mrefu kwa wananchi wa Syria.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, Katibu Mkuu amesema kuwa “sote tunatambua kuendelea kuibuka kwa janga kaskazini-magharibi mwa Syria na idadi kubwa ya vifo vya raia. Takribani watu 900,000, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto, wamekimbia mapigano ya hivi karibuni wakiwa katika mazingira magumu. Mamia wameuawa. Wengi wao wameshakimbia mara kadhaa.”

Katibu Mkuu amesema watoto wanaganda na kufariki dunia kutokana na baridi kali na kwamba mapigano hivi sasa yanafanyika kwenye maeneo ya raia wengi, ikiwemo kwa wakimbizi na kusambaratisha njia za usafirishaji wa misaada ya kibinadamu.

Kama hiyo haitoshi, amesema, sheria ya kimataifa ya kibinadamu na ulinzi wa raia zimepuuzwa na maeneo salama ya raia yanazidi kubinywa huku fursa kwa watu kupata machungu zaidi ikiongezeka.

Idadi  ya wanaohitaji misaada

Bwana Guterres amesema kuwa takribani watu milioni 2.8 kaskazini-magharibi mwa Syria wanahitaji misaada ya kibinadamu.

“Mapema mwezi huu, tulitarajia kuwa pengine tungalifikishia misaada watu 800,000 waliosambaratishwa na ghasia hivi karibuni. Tunabadili mipango yetu na tunatoa ombi kwa wahisani la nyongeza ya dola milioni 500 kukidhi mahitaji ya wakimbizi wapya kwa ajili ya kuwasaidia kwa miezi sita ijayo,” amesema Bwana Guterres.

Mtoto akitembea kwenye theluji katika makazi ya muda ambayo yanawahifadhi wakimbizi wanaokimbia machafuko kusini mwa Idlib na Aleppo vijijini, Syria.
© UNICEF/Baker Kasem
Mtoto akitembea kwenye theluji katika makazi ya muda ambayo yanawahifadhi wakimbizi wanaokimbia machafuko kusini mwa Idlib na Aleppo vijijini, Syria.

Mapigano  yanafanya hali kuwa mbayá zaidi

Katibu Mkuu amesema hali  ya  kibinadamu ikizidi kuwa mbaya, kile kinachoendelea sasa kina hatari zaidi hususan huko Idlib ambako amesema, “eneo la kutokuwepo kwa mapigano huko Idlib lilianzishwa mwaka 2017 na pia kupitia makubaliano kati ya Urusi na Uturuki ya Septemba mwaka 2018 huko Sochi. Hata hivyo mwishoni mwa mwezi Februari mwaka jana, mpango huo ulianza kusambaratika, licha ya masitisho ya mara kwa mara ya mapigano. Kwa takribani mwaka mmoja sasa, tunashuhudia mashambulizi yanayofanywa na jeshi la Syria kwa kuungwa mkono na Urusi.”

Jeshi la Uturuki nalo mwezi huu limekuwa likipambana na jeshi la Syria ikimanisha kuwa hali ya kibinadamu inazidi kuwa  mbaya “na kila mara nimekuwa nikitaka sitisho la mapigano Idlib ili kumaliza janga la kibinadamu na sasa tena ili kuepusha kuendelea kwa mapambano.,”

Bwana Guterres amesema amepeleka ujumbe huo hadharani na pia moja kwa moja kwa wahusika huku mjumbe wake maalum kwa Syria na mratibu wa masuala ya dharura wakitoa taarifa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu amesema, “ujumbe wangu ni dhahiri. Hakuna suluhu ya kijeshi Syria. Suluhu pekee iliyosalia ni ya kisiasa. Janga hili lililoanzishwa na binadamu lazima likome na likomesa sasa.”

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter