Guterres apongeza makubaliano kati ya Uturuki na Urusi kuhusu Idlib

Msichana wa umri wa miaka saba asimama mbele ya jengo la shule lililoharibiwa  mjini Idlib Syria.
UNICEF
Msichana wa umri wa miaka saba asimama mbele ya jengo la shule lililoharibiwa mjini Idlib Syria.

Guterres apongeza makubaliano kati ya Uturuki na Urusi kuhusu Idlib

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likikutana leo mjini New York, Marekani kujadili hali ya kisiasa na kibinadamu nchini Syria, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekaribisha makubaliano kati ya marais wa Uturuki na Urusi kuhusu kutenga eneo lisilo la mapigano huko Idlib nchini Syria.

Makubaliano hayo yalifikiwa tarehe 17 mwezi huu wa Septemba kati ya Rais Tayyip Erdogan wa Uturuki na Vladmir Putin wa Urusi na hivyo kuleta nuru kwa wakazi wa eneo hilo ambao kwa miezi kadhaa sasa wamekuwa wahanga wa makombora yanayorushwa na serikali ya Syria ikisema inalenga wapiganaji wanaoipinga.

Eneo hilo lisilo la mapigano litakuwa halihusishwi na operesheni za kijeshi ambazo zimekuwa zikiendelezwa na Syria na wadau wake kwenye eneo hilo la Idlib na kusababisha vifo vya maelfu ya raia na uharibifu wa miundombinu.

Bwana Guterres katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake amesema hatua hii ya makubaliano itaepusha zahma dhidi ya mamilioni ya raia wa Syria.

 

Image
Wavulana wawili wakipita karibu na maghofu huko Idlib Syria.(Picha:UNICEF/Giovanni Diffidenti)

Katibu Mkuu ametoa wito kwa pande zote kwenye mzozo wa Syria kushirikiana na kutekeleza makubaliano hayo na kuhakikisha kuna njia salama na za moja kwa moja zisizo na vipingamizi ili kufikisha misaada ya kibinadamu kwa raia.

Halikadhalika amesisitiza umuihmu wa kuchukua hatua haraka kusaka mzizi wa mzozo unaoendelea na kupitisha suluhu ya kudumu ya kisiasa kwa mujibu wa azimio namba 2254 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.