Wanawake Syria wanakaa wiki kadhaa bila kuoga kwa kuhofia usalama wao-OCHA

13 Machi 2020

Vurugu zimepungua huko Idlib kwenye eneo linalopaswa kutokuwepo kwa mapigano nchini Syria kufuatia tangazo la Urusi na Uturuki la kusitisha mapigano.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, Jens Laerke amesema uhasama umepungua na mashambulizi ya anga yamesitishwa huku ufurushwaji katika maeneo hayo pia umepungua.

Hatahivyo bwana Laerke ameonya kwamba Idlib sio mahali salama bado kwani hali kaskazini magharibi inasalia kuwa mbaya ikiashiria hali tete ya mzozo wa Syria wakati mzozo ukiingia mwaka wa kumi.

OCHA imesema mahitaji ya kibinadamu yanasalia kuwa makubwa huku takriban watu 960,000 wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake wamefurushwa makwao tangu Desemba.Watu 327,000 kwa sasa wanaishi katika kambi na mahema binafsi huku wengine 165,000 wako katika nyumba au majengo ambayo hayajakamilika kukarabatiwa.

Wakimbizi wa ndani 366,000 wanaishi na familia zinazowahifadhi au katika nyumba za kukodi huku watu 93,000 wanaishi katika makazi ya pamoja yaliyokuwa shule aua misikiti huku wengine wakilazimika kusaka hifadhi chini ya miti.

Kwa mujibu wa OCHA, wafanyakazi mashinani wanaelezea athari za vita kwa wanawake na wasichana ambapo watu wanne kati ya watano waliolazimika kukimbia makwao tangu Desemba mosi ni mwanamke, msichana au mvulana, ambao afya yao, usalama na uzima uko hatarini.

Aidha wafanyakazi wanaripoti matukio ya kutumiwa vibaya na ukatili dhidi ya wanawake wakimbizi na wasichana na wanaume walio katika nafasi za mamlaka kwa mfano wamiliki wa majengo kwa ajili ya kupata pesa au msaada wa bidhaa.

Kuna ripoti pia za wanawake kushindwa kuoga kwa wiki nyingi kwa sababu ya kukosa faraga na kujinyima chakula na maji na chakula ili wasiende kwa choo kwani wanahisi hawako salama. Pia machafuko yameathiri wanawake wanaonyonysha na kusababisha ongezeko la watoto kudumaa kutokana na utapiamlo.

Kwa mantiki hiyo Umoja wa Mataifa umeiongeza juhudi za msaada ka ajili ya kukabiliana na hali kwa kuwaslisha msaada wa chakula, makazi, maji, bidhaa za kujisafi na usafi.

Umoja wa Mataifa umeoa wito kwa pande husika kuhakikisha ulinzi wa raia na miundombinu ya raia kwa mujibu wa sharia za kimataifa za binadamu na kuhakikisha ufikiaji wa waathirika wa mzozo na misaada ya kibinadamu.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter