Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yajizatiti kukabiliana na taarifa potofu kuhusu virusi vya corona, Guteress aonya kuhusu unyanyapaa

Wafanyakazi wa uwanja wa ndege wa Chengdu Shuangliu nchini China.
UN News/Jing Zhang
Wafanyakazi wa uwanja wa ndege wa Chengdu Shuangliu nchini China.

WHO yajizatiti kukabiliana na taarifa potofu kuhusu virusi vya corona, Guteress aonya kuhusu unyanyapaa

Afya

Shirika la Afya Ulimwenguni, WHO limechukua hatua kuhakikisha kuwa janga la virusi vya corona ambalo limesababisha vifo vya mamia ya watu katikati mwa China halitachangia kuchochewa kwa taarifa potofu kwenye mitandao ya kijamii.

Na wakati huu kukiwa na wasiwasi kwamba watu wa asili ya China wanabaguliwa kutokana na hofu ya kuenea kwa ugonjwa huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres ametoa wito wa mshikamano wa kimataifa na kukomesha ubaguzi wowote kwa waathirika wa virusi hivyo.

Kuhusu wingu la maambukizi

Mkurugenzi wa WHO anayehusika na maandalizi ya magonjwa ya kuambukiza kimataifa, Sylvie Briand, amewaambia waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi Jumanne kwamba shirika hilo tayari limejizatiti kumaliza uvumi wa mtandaoni kwamba virusi vinaweza kusambaa kutoka kwenye "wingu" la kuambukiza.

Dkt. Briand amesema, "watu walikuwa na dhana kwamba virusi vipo angani na ... kuna wingu la virusi" ambalo linaweza kusababisha maambukizi. "Hii sio hali ilivyo. Hivi sasa virusi huambukizwa kupitia matone na unahitaji ushirikiano wa karibu ili kuambukizwa.. Kwa hivyo tunajaribu kufafanua kile tunachojua kuhusu virusi hivyo kisayansi - ambavyo bado havijulikani - na kutoa maoni ambayo yanaweza kusaidia watu kujilinda na kulinda familia zao. "

Kufikia leo watu 425 wamepoteza maisha kwa mujibu wa WHO na kuna zaidi ya visa 20,000 vilivyoripotiwa nchini China na visa 158 nje ya nchi.

Katika ombi la kutaka ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na mlipuko huo, Dkt. Briand amesema ni muhimu kutobinya taarifa lakini kutoa taarifa sahihi kuhusu kile ambacho kinafahamika kuhusu virusi hivyo na kile kisichojulikana.

Amesema kuwa wale walio hatarini zaidi ni wale walio na kinga dhaifu kwa sababu ya magonjwa mengine kama saratani na mengine ya muda mrefu, na wazee.

Ni mapema sana kutathmini tishio kamili

Dkt. Briand ameongeza kuwa ni mapema sana kutathmini kuhusu hatari ya virusi ilivyo, akisisitiza tena ushauri wa WHO wa kunawa mikono na kuvaa vifaa vya kujikinga na maambukizi wakati unawasiliana na watu walioambukizwa.

Akiangazia utayari wa mamlaka ya China kukabiliana na mlipuko huo, Dk Briand amesema kuwa wanasayansi walikuwa na ari ya kupata habari zaidi juu ya wale waliokufa.

Kwani hii itasaidia kuelewa sababu ya msingi ya hali ya kiafya ambayo inaweka watu katika hatari, na kuongeza kuwa watafiti kwa sasa wanawazingatia wanawake wajawazito na watoto wadogo kuona ikiwa mifumo ya maambukizi ni sawa na ya mafua.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akizunugmza na waandishi wa habari jijini New York Marekani.
UN Photo/Mark Garten)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akizunugmza na waandishi wa habari jijini New York Marekani.

Guterres atoa wito wa kuunga mkono China na mataifa mengine

Katika mkutano na waandishi wa habari kwenye Makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani Jumanne, Katibu Mkuu wa Umoja  wa Mataifa António Guterres amesema WHO iliamua kutangaza dharura ya afya ya ulimwengu kuhusu virusi vya corona wakati unaofaa" na wamekuwa mstari wa mbele kuunga mkono China na mataifa mengine yanayokabiliwa na mlipuko.

Ameongeza kwamba, “tunajaribu kuhamasisha uwezo wetu bora na rasilimali bora" , na kuongeza kuwa hakuna mfanyikazi wa Umoja wa Mataifa ambaye ameambukizwa hadi sasa.

Ametoa wito,  wa“mshikamano wa kimataifa thabiti na kuunga mkono China wakati huu mgumu na nchi zote ambazo huenda zikaathiriwa”, huku akielezea , “wasiwasi mkubwa kuzuia unyanyapaa wa watu ambao hawana hatia, na waathirika wa hali hiyo."