Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dunia inapungukiwa vifaa vya kujikinga wakati idadi ya waathirika wa corona ikipanda-WHO

Watu wakiwa wamevaa vifaa vya kinga kwenye duka mji wa mashariki mwa China, Nanjing.
UN News/Li Zhang
Watu wakiwa wamevaa vifaa vya kinga kwenye duka mji wa mashariki mwa China, Nanjing.

Dunia inapungukiwa vifaa vya kujikinga wakati idadi ya waathirika wa corona ikipanda-WHO

Afya

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus ameonya kuwa ulimwengu unakabiliwa na sintofahamu kubwa katika soko la vifaa vya kujikinga na kutoa wito kwa nchi na makampuni kufanya kazi na WHO "kuhakikisha matumizi sawa ya vifaa na kuzingatia mizania katika soko" katika kukabiliana na virusi vipya vya corona (2019-nCoV).

Akizungumza na waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi hii leo, Dk Tedros amesema "WHO inakataza uwekaji wa vifaa vya kujikinga katika nchi na maeneo ambamo visa vya maambukizi viko chini," akiongeza kuwa shida nyingine inahusiana na kwamba, "wakati idadi ya vifaa ni ndogo na mahitaji ni mengi, basi kuna uwezekano wa watu kuficha vifaa hivyo kwa minajili ya kuziuza kwa bei ya juu.”

Ameongeza kwamba, "ndio sababu tunataka mshikamano. Na kwa watu kuelewa mapambano kama ya virusi vya corona ni nini. Na kuunga mkono usalama wa binadamu badala ya wao kutafuta faida zao. Kwa hivyo kuna suala la maadili hapa pia, na ndiyo sababu tulikuwa na mazungumzo na wazalishaji na wengine pia, ili kushirikiana, na natumai watasimama pamoja kwa msinig wa kuonesha mshikamano. "

Kwa upande wake Dk Mike Ryan kutoka WHO mtaalamu wa Programu ya afya na dharura amesema, "sio wazalishaji tu, ni wazalishaji wa malighafi. Ni wazalishaji, ni wasambazaji, wauzaji wa jumla, na wauzaji. Kwa sababu katika kila hatua ya usambazaji, kuna uwezekano wa usumbufu, au faida, au bidhaa kupelekwa kwingine. "

Ameongeza kwamba, "Kwa hivyo hii sio shida rahisi kutatua. Kuna wadau wengi, kwa umma na kwenye sekta binafsi. Tunahitaji mshikamano sio tu kati ya nchi, lakini tunahitaji mshikamano wa kina kati ya umma na sekta binafsi kuhakikisha kuwa hatufiki hatua ambayo wafanyikazi wa afya wanalazimika kuwatunza wagonjwa bila vifaa vya kinga. "

Kwa mujibu wa WHO leo Januari 7 kuna visa 31,211 zilizothibitishwa nchini China, na vifo 637. Nje ya China, kuna visa 270 katika nchi 24, na kifo 1.