Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maelfu wafungasha virago kukimbia machafuko mapya Darfur:UNHCR

Mtazamo wa mji wa El Geneina, mji mkuu wa Darfur magharibi, Sudan.
UNAMID/Hamid Abdulsalam
Mtazamo wa mji wa El Geneina, mji mkuu wa Darfur magharibi, Sudan.

Maelfu wafungasha virago kukimbia machafuko mapya Darfur:UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Machafuko yanayoendelea El Geneina kwenye jimbo la Darfur Magharibi yamewalazimisha watu Zaidi ya 11,000 kukimbilia nchi jirani ya Chad kama wakimbizi limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo mjini Geneva Uswis watu 4000 miongoni mwa idadi hiyo wamekimbia wiki iliyopita pekee na inakadiriwa kwamba mapigano hayo mapya yamewatawanya watu wengine 46,000 ndani ya Sudan.

Idadi kubwa ya watu hao tayari walikuwa wakimbizi wa ndani na mashambulizi mapya yalipozuka Darfur Magharibi mwezi Desemba mwaka 2019 ikiwemo ndani ya kambi ya wakimbizi wa ndani walifungasha virago na kukimbia kupata hifadhi mashuleni, misikitini, na katika majengo mengine El Geneina. Babar Baloch ni msemaji wa UNHCR Geneva,“El Geneina ikiwa kilometa 20 tu kutoka mpakani , maelfu ya wakimbizi wamevuka mpaka na kuingia Chad na UNHCR inakadiria idadi yao kufikia 30,000 katika wiki chache zijazo kwani machafuko yanaendelea. Timu za UNHCR zilizoko huko zinasikia watu wakisema walikimbia baada ya vijiji vyao, nyumba zao na mali zao kushambuliwa na nyumba nyingi kuteketezwa kwa moto kabisa.”

Ameongeza kuwa nchini Chad wakimbizi hao hivi sasa wametawanyika katika vijiji mbalimbali  ikiwemo katika mji wa Adre kwenye ji,mbo la Ouaddai ambalo tayari linahifadhi wakimbizi wa Sudan kusini 128,000.

UNHCR inasema hali ni mbayá na wengi wa wakimbizi hao wanaishi katika maeneo ya wazi au kwenye mahema bila ulinzi wa kutosha. Na mahitaji ya msingi kama maji na chakula ni haba hivyo yanahitajika haraka huku hali ya afya ikitia wasiwasi.

UNHCR, serikali na wadau wengine wa misaada ya kibinadamu wako katika maeneo husika kuratibu misaada, kuorodhesha wakimbizi na kuwapa msaada wa lazima kama chakula , maji  na kuna wakimbizi wanaohitaji huduma maalum wakiwemo watoto.