Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS na serikali Sudan Kusini wakabiliana na wizi wa mifugo

Wafugaji wakiswaga mifugo yao kusaka maji huko Darfur nchini Sudan,
UNAMID/Albert González Farran
Wafugaji wakiswaga mifugo yao kusaka maji huko Darfur nchini Sudan,

UNMISS na serikali Sudan Kusini wakabiliana na wizi wa mifugo

Amani na Usalama

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kuisni, UNMISS kwa kushirikiana na mamlaka nchini humo katika juhudi za pamoja wamezindua kampeni ya kuchagiza amani wakilenga wamiliki wa mifugo waliojihami katika kambi katika baadhi ya maeneo.

Video ya UNMISS ikionyesha wafugaji na mifugo yao, wakitembea, huku mkononi wamebeba bunduki. Wakazi katika kambi hii ya mifugo eneo la ziwa nchini Sudan Kusini wanajivunia kumiliki mifugo wengi.

Wengi wa wafugaji hubeba bunduki zisizo halali kwa ajili ya kulinda mifugo yao, ambazo hutembea nazo bila kuficha. Katika kambi ya mifugo ya Aguoc, ambayo ni kambi kubwa zaidi eneo la ziwa kwa vijana leo ni siku njema.

Wamealikwa katika tukio la amani pamoja na wafugaji majirani wengine jirani zao. Katika kitendo cha kitamaduni cha kuja pamoja na baada ya salamu wako tayari kuanza shughuli zao za siku.

Wageni hawa wamekuja kwa ajili ya kuleta amani na kuacha mashambulizi dhidi ya wale wanaoishi kambi ya mifugo ya Aguoc. Matumini yao ni kuunda ushirikiano na kukomesha mzunugko wa vitendo vya kushambuliana na kulipizana kisasi kati ya makundi hayo.

Dut Mariel, ni mfugaji kutoka eneo la Panyar, « Jinsi watu walivyohamia katika eneo hili lenye unyevunyevu hapakuwa na mpangilio. Wengine wetu hatujatoka sehemu hii, tulikuja kwa sababu wale wa eneo la Lieth na Jath kutoka jamii ya Rup kwa sasa wanakalia ardhi yetu Marialbek. Kadri wanavyokalia ardhi yetu hakutakuwa na kuishi pamoja kwa usalama. »

Kampeni hizi za amani zimekuja wakatika mzuri kwani zinalenga kukabiliana na dalili za mapema za mzozo kabla ya msimu wa ukame ambao ni wakati hatari kwa wizi wa mifugo, mauji ya kulipiza kisasi na mgogoro juu ya malisho na maji kwa ajili ya matumizi ya mifugo na binadamu. Gibril Allan Turay, ni afisa wa masuala ya umma, wa UNMISS, “Ili kutatua mizozo hii, tuligundua kwamba tunahitaji kutoa elimu kwa jamii hususan katika kambi za mifugo ambako pigo kubwa la ukatili lipo. Kwa sababu ni huko kambini ambako kuna vijana waliobeba bunduki na risasi na wao ndio wanasababisha mvutano katika jamii. »

Lakini sio tu kwamba wizi wa mifugo unaathiri wanaume na vijana lakini pia wanawake. Mayen Kuluel, ni mwanamke anayeishi katika kambi ya mifugo ya Agouc, “Wakati mapigano yanazuka, wanawake wanabakwa kwa sababu wanaume ambao wangewalinda wamekwenda kwenye uwanja wa vita. Kama hiyo haitoshi tumepoteza wavulana wetu katika migogoro hiyo. Wanawake wengi wa umri wangu sasa hivi hawana watoto  na ni wajane.”

UNMISS inatarajia kuendesha kampeni za aina hiyo katika kambi zingine nchini humo.