Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tumeambiwa kuna amani, basi turejee nyumbani-mkimbizi wa ndani Sudan Kusini

Kijiji nchini Sudan Kusini, barabarani kati ya Yambio na Maridi, Equatoria ya Magharibi.
UN Photo/JC McIlwaine
Kijiji nchini Sudan Kusini, barabarani kati ya Yambio na Maridi, Equatoria ya Magharibi.

Tumeambiwa kuna amani, basi turejee nyumbani-mkimbizi wa ndani Sudan Kusini

Amani na Usalama

Hali ya utulivu imerejea kwa kiasi fulani kufuatia mashambulizi katika kijiji cha Rimenze ambako watu wanne walitekwa huku maelfu wakikimbia kwenda kujificha vichakani baada ya watu waisojulikana kushambulia kanisa lililoko vitongoji vya mji wa Yambio kusini magharibi mwa Sudan Kusini.

Wenyeji hao ambao ni takriban watu elfu tatu waliokimbia vijiji vyao na wamekuwa wakiishi katika uwanja wa kanisa hilo tangu kuzuka kwa mzozo mika mitatu iliyopita bado wako katika hali ya wasiwasi na wameelezea kilichotokea baada ya nyumba zao kuteketezwa kwa moto na mali zao kuharibiwa au kuibiwa na watu waliojihami kwa silaha na wasiojulikana.

Charles Jacob Mbaro muathirika na  mmoja wa wakimbizi wa ndani Rimenze“Waliezua nyasi kutoka kwenye kibanda changu na kuziteketeza, alafu wakaingia katika kibanda cha jirani yangu na kupora baiskeli, piki piki na paundi 30,000 za Sudan Kusini ambazo ni sawa na dola 300 za Marekani kisha wakaondoka.”

Awali wakimbizi hao waliogopa kurejea nyumbani kwao na sasa shambulio hilo limewaacha na wasiwasi zaidi wakati huu ambapo muda wa kuundwa kwa serikali ya pamoja ya umoja wa kitaifa umeongezwa kwa siku mia moja kuanzia Novemba 12, huku wengi wakiachwa na sintofahamu ya muda wa kurejea nyumbani kwao. Maria Raphael ni mkimbizi wa ndani.

“Wanatuambia kuna amani, basi turejee nyumbani, lakini tunaambiwa kwamba mchakato umesongeshwa hadi , miezi mitatu au minne. Na  tayari tulikuwa tunaanda nyumba kwa ajili ya watoto wetu na tulikuwa tunapanga kulima mazao kwa matumaini kwamba kutakuwepo amani, lakini bila amani tutasalia hapa kambini.”

Timu ya pamoja ya kutathmini imepelekwa Rimenze kutoka kwenye Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS ikiwemo masuala ya haki za binadamu, ulinzi wa watoto na masuala ya raia kwa ajili ya kuzungumza na watu mashinani. Antonina Okuta ni afisa wa haki za binadamu kutoka UNMISS.

“Raia hawapaswi wakati wowote ule kuwa katika mazingira kama hayo. Wanahitaji kufurahia haki zao, iwe ni kwenye mzozo au wakati wa amani, Na sasa katika tukio hili ambapo wananchi wako katika uwanja wa kanisa Rimenze, katika sehemu ambapo wamekuja kujihifadhi na wanashambulia na kuteketezwa vibanda vya raia, ni hali mbaya.”

Timu imetoa pendekezo kwa mamlaka ya taifa kuweka kituo cha polisi Rimenze ili kuweza kuzuia baadhi ya matukio yanayoathiri eneo hilo.