Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ILO imechukua hatua kurahisisha upatikanaji wa vibali vya kazi kwa wakimbizi nchini Jordan

Kikundi cha wanawake kutoka Syria na Jordan kimepatiwa msaada na shirika la kazi duniani, ILO na kuanzisha biashara ya pamoja ya kuuza vitamutamu na vyakula huko Jordan.
ILO Video
Kikundi cha wanawake kutoka Syria na Jordan kimepatiwa msaada na shirika la kazi duniani, ILO na kuanzisha biashara ya pamoja ya kuuza vitamutamu na vyakula huko Jordan.

ILO imechukua hatua kurahisisha upatikanaji wa vibali vya kazi kwa wakimbizi nchini Jordan

Ukuaji wa Kiuchumi

Nchini Jordan shirika la kazi duniani, ILO limechukua hatua kurahisisha wakimbizi kutoka Syria wanaofanya kazi kwenye sekta ya kilimo na ujenzi wanapata vibali vya kazi kwa njia rahisi zaidi tofauti na sasa. 

Nchini Jordan, Mustafa Hassan mmoja wa wakimbizi kutoka Syria akiwa katika kazi yake ya ufundi uashi ambayo ni muhimu ili kusaidia familia yake ya watu wanane.

Hadi hivi karibuni ilikuwa vigumu sana kwake yeye aishie kijijini kupata ajira kutokana na umbali aliko na gharama za usafiri za kumfikisha maeneo ya kupata kibali cha kazi.  

 (Sauti ya Mustafa)

 “Tulikuwa tunapata vibali  vya kazi kupitia vyama vya ushirika. Tulipaswa kuchukua likizo ya siku moja ili kwenda ofisi ya ajira kujaza nyaraka za kibali. Na yeyote aliyekuwa anatusaidia naye alilazimika kuchukua siku moja ya mapumziko.”

 Zahma hiyo iliyomkumba Mustafa na wenzake hatimaye ilipatiwa suluhu baada ya shirika la kazi duniani ILO nchini Jordan kuandaa gari linalotembea sehemu moja hadi nyingine kutoa huduma za kupatia vibali vya kazi wakimbizi kutoka Syria.

ILO imeshirikiana na vyama vya ushirika vya kilimo na shirikisho la vyama vya wafanyakazi Jordan kusaidia wafanyakazi kwenye sekta ya kilimo na ujenzi katika maeneo ya Irbid na  Zarqa.

 Nats..

Sasa magari mawili  yaliyogeuzwa ofisi hutembelea wafanyakazi kwenye maeneo ya ndani zaidi ya Jordan na kuwawezesha wafanyakazi hao kuomba vibali vipya au kuongeza muda wa vibali vya kazi vilivyomalizika  muda hapo walipo na bila gharama  yoyote.

(Sauti ya Mustafa)

 “Gari hilo linalotoa huduma za vibali limefika hapa na kuchukua nyaraka zangu na baada ya kuonekana muda wa kibali umemalizika niliweza kupata kibali kipya kupitia gari hili. Sikulazimika kuchukua siku ya mapumziko mimi wala wafanyakazi wengine hapa.

ILO inatumai kuwa katika awamu ya pili ya mradi huu itaelekeza majimbo mengine na kufikia wafanyakazi zaidi walio maeneo ya ndani zaidi.