Wafanyakazi wa mashambani Jordan ni taabani- ILO

26 Novemba 2018

Utafiti uliofanywa na shirika la kazi duniani, ILO huko Jordan, umebaini kuwepo kuwa wafanyakazi wa mashambani hususan wakimbizi kutoka Syria wanaoishi nchini humo wanafanya kazi katika mazingira magumu na hivyo hatua zinapaswa kuchukuliwa kuwaokoa.

Nchini Jordan katika moja ya mashamba ya mizeituni, uvunaji wa zeituni ukiendelea na Mohammed Hassan Al Ali mkimbizi kutoka Syria anasimulia.

“Nilikuja huku Jordan mwaka 2013 na kuanza kufanya kazi mashambani. Nchini Syria nilikuwa mkulima na nina uzoefu wa kilimo”

Hali ya maisha ni ngumu hivyo Mohammed anasema hata watoto wake wawili wamelazimika kuacha shule ili wafanye kazi shambani kwa lengo la kuinua kipato cha familia.

ILO inasema utafiti uliohusisha wafanyakazi wa mashambani wenye vibali ulibaini kuwa kuna mazingira magumu ya kazi ikiwemo  malazi duni, vifaa duni vya kazi na zaidi  ya yote anafafanua Maha Kattaa, afisa wa ILO kanda ya Mashariki ya Kati ….

“Hali ni mbaya hasa katika suala la utumikishaji watoto kwenye sekta hii.”

Katika video hii ya ILO kuhusu hali ya watumishi mashambani, wanaonekana watoto wakiwa wamebeba makasha yenye mavuno ya mboga, ambapo mmiliki mmoja wa shamba anasema wazazi ndio wanashinikiza watoto wao wafanyishwe kazi na iwapo wakifanya wakichoka wanawapatia siku ya kupumzika.

Hata hivyo ili kuondokana na kitendo cha utumikishaji watoto mashambani na ajira katika mazingira magumu mashambani, Tamer Awawdeh, mkaguzi wa kazi huko Irbid, anasema..

Kwa maoni  yangu, kuongeza uelewa miongoni mwa wafanyakazi kuhusu haki zao ndio njia fanisi ya kuboresha mazingira ya kazi. Wafanyakazi watambue haki na wajibu wao.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa COP26 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter