Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoka Chuo Kikuu hadi kuondoa maotea kwenye mizeituni, asante ILO- Mkimbizi 

Zao la mizeituni
Maha Kadadha
Zao la mizeituni

Kutoka Chuo Kikuu hadi kuondoa maotea kwenye mizeituni, asante ILO- Mkimbizi 

Wahamiaji na Wakimbizi

Nchini Jordan changamoto ya wananchi, wakimbizi na hata wahamiaji kupata ajira imepata suluhisho baada ya shirika la Umoja wa Mataifa la kazi ulimwenguni, ILO, kuingia ubia na vyama vya ushirika vya kilimo wa kuunganisha wasaka ajira na wamiliki wa mashamba

Kazi ya kuondoa maotea kwenye miti ya mizeituni ikiendelea nchini Jordan na afanyaye kazi hiyo ni mkimbizi kutoka Syria Safwan Raslan ambaye anasema, “kama wasyria, hatuwafahamu wamiliki wa mashamba na kazi hapa ni ya msimu. Kwa hiyo kupitia vitengo vya ajira, wanatutafuta wakitupata tunakwenda kufanya kazi.” 

Vitengo vya ajira anavyoelezea viko sita na viliundwa ndani ya vyama vya ushirika kwa usaidizi wa ILO

Miongoni mwa vyama hivyo ni kile cha Kufr Sum  klichomsaidia pia raia wa Jordan Sameh Obaidat kupata kazi shambani ambako anapunguza matawi ya mizeituni. 

Sameh anasema, “kama raia wengine wa Jordan nimeshindwa kupata kazi ya kile nilichosomea. Nimehitimu Chuo Kikuu katika fani ya mifumo ya kompyuta. Lakini Kufr Sum walichukua taarifa zetu na sasa kuna kiunganishi kati ya waajiri na waajiriwa na kuna fursa za kazi.” 

Amal Rosan, mmiliki wa shamba la mizeituni anasema sasa hali ni shwari.

“Kabla ya vitengo vya ajira kwenye ushirika, ilikuwa vigumu kupata wafanyakazi kwenye mashamba, ilikuwa kupitia mtu binafsi tu. Lakini sasa ukitaka wafanyakazi  20 unaletewa hata ukitaka 30. Tukitaka wale wenye ujuzi tunaletewa pia, hali imebadilika.” 

Pamoja na kuwezesha kupata ajira, vitengo hivyo vinasaidia wakimbizi kupata vibali vya kazi na  hivyo wakimbizi wanapata kipato badala ya kuwa tegemezi. 

Faida nyingine ni wafanyakazi wanapata mafunzo ya stadi za kilimo ambapo Amira Obaidat mkimbizi kutoka Jordan anasema, “wametufundisha kuondoa maotea na magugu. Na iwapo mti una ugonjwa tunajua la kufanya.Vitengo vya ajira vimefungua njia kwani waliokuwa hawana ajira sasa wana ajira. Mfano mimi, nimehitimu chuo lakini nilikuwa sifanyi kazi. Kama mwanamke sikutarajia kuwa ningalifanya kazi ya kuondoa maotea na kulima.”