Vikosi vya upinzani Sudan Kusini vyaanza kujumuishwa kwenye jeshi la kitaifa

23 Januari 2020

Hatimaye mpango wa kujumuisha vikosi vya upinzani kwenye jeshi la Sudan Kusini umeanza kutekelezwa ikiwa ni katika kutekeleza makubaliano mapya ya amani yaliyotiwa saini mwezi Septemba mwaka 2018.

Utekelezaji umeanza katika jimbo la Equatoria Magharibi na kushuhudiwa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini David Shearer ambapo maadui hao wa muda mrefu sasa wanakuwa marafiki na kufanya kazi katika jeshi moja la kitaifa.

Wanajeshi hao wa upande wa upinzani wapatao 500 wamekuwa wakisubiri katika kambi ya Sue jimboni humo ili waweze kusafirishwa kwenye kambi ya pamoja ya mafunzo iliyopo eneo la Maridi ambako wataungana na wanajeshi wengine 500 wa Brigedi ya 16 kutoka jeshi la ulinzi la Sudan Kusini.

Kamanda wa Brigedi hiyo ya 16 ya jeshi la Sudan Kusini Jenerali Jordan Oting amezungumzia hatua hiyo akisema ya kihistoria na kwamba, “Vikosi vya jeshi la ulinzi la Sudan Kusini, SSPDF kwa kweli vimepokea hatua hii kama wito wa kitaifa. Wito wa taifa ni wajibu wetu na ni jukumu kwa SSPDF kuona hili kama jukumu letu na utashi wa kupanga upya SSPDF kwa ajili ya heshima ya taifa hili, kwa ajili ya ulinzi wa taifa hili hususan katiba ya taifa.”

Ingawa uamuzi wa kuunganisha vikosi vya ulinzi vya upinzani na jeshi la taifa ni sehemu ya makubaliano yam waka 2018, bado mchakato huu umekuwa na changamoto dhahiti kama alivyoelezea Bwana Shearer ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS akisema, “kimsingi kuna masuala mawili. Mosi ni utashi wa kisiasa—utashi wa viongozi na pia wanajeshi wenyewe kukubali vikosi vyao viingie kambini na pia katika maeneo ya mafunzo. Lakini hilo ni moja. Pili ni kuhakikisah kuwa wana vifaa vinavyotakiwa na rasilimali muhimu. Wakati mwingine fedha zinazotengwa hazitoshi, maeneo mengine kuna  uhaba wa chakula. Kunatakiwa mkakati bora zaidi wa kuhakikisha kuwa maeneo wanakopelekwa yana rasilimali zinazotakiwa ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.”

Rasilimali hizo ni pamoja na kuhakisha maeneo ya kambi na mafunzo yana maji salama, vyakula, dawa na malazi. UNMISS inasema kuwa suala hilo linatia hofu zaidi kwa sababu familia nyingi huambatana na askari hao hadi maeeneo ya kijeshi.

Hata hivyo licha ya changamoto hizo Bwana anaona kuna nuru zaidi akisema kuwa, “hebu ona ni muhimu sana kuwa vikosi hivi vinashirikiana. Lakini hawawezi kuwa pamoja ndani ya usiku mmoja. Hebu tutambue kuwa wamekuwa wapinzani wakipiana miaka yote na kutarajia kuwa waelewane ndani ya usiku mmoja au ghafla tu hili si uhalisia. Lakini ni mchakato na kadri kuna kujengeana imani miongoni mwa viongozi na watu wakiona kuwa wanapelekwa kambini, na pia wote wavae sare moja na hatimaye kupelekwa lindoni pamoja, hii itawapatia imani kutambua kuwa taifa hilo liko kwenye mwelekeo wa kusonga mbele.”

Kuungainshwa kwa vikosi hivi kulipaswa kuwe kumekamilika kabla ya kuundwa kwa serikali mpya ya mpito.

Hata hivyo UNMISS inasema kuwa hilo linaweza lisitimie kufikia ukomo wa tarehe 22 mwezi ujao wa Februari, tarehe ambayo ilikubaliwa na pande zote.

 

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter