Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua ya viongozi wa Sudan Kusini kuweka maslahi ya nchi mbele inatumainisha- Shearer

Baraza la Usalama lakutana kuhusu Sudan Kusini ambako mwakilishi wa UN nchini humo amehutubia kwa njia ya video
UN Photo/Eskinder Debebe)
Baraza la Usalama lakutana kuhusu Sudan Kusini ambako mwakilishi wa UN nchini humo amehutubia kwa njia ya video

Hatua ya viongozi wa Sudan Kusini kuweka maslahi ya nchi mbele inatumainisha- Shearer

Amani na Usalama

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudani Kusini David Shearer amesema hatua kuelekea mchakato wa amani nchini humo zimepigwa kufuatia, "utayari wa kisiasa wa watu wawili ambao wameweka mbele matakwa ya nchi yao ."

Akihutubia Baraza la Usalama kwa njia ya video hii leo, Bwana Shearer amesema, "mara nyingi tunazungumza juu ya ujasiri katika mapigano na vita. Lakini kusaka amani pia kunahitaji ujasiri.”

Mwakilishi huyo maalum ameangazia hatua chanya ambazo zimesogeza nchi hiyo changa zaidi duniani katika barabara kuelekea amani endelevu kutokana na u tayari kisiasa wa Rais Salva Kiir na Makamu wake wa zamani Riek Machar kwa kuweka maslahi ya nchi yao kwanza katika makubaliano ya serikali ya mpito.

Amesema hatua hiyo imeibua hisia za utulivu kote nchini, huku makubaliano yakiwa ni kipaumbele ni kuunda serikali ya mpito ili makubaliano ya amani na nchi yaweze kusonga mbele.  

Amesema kwamba pande husika wanafanya mazungumzo juu ya ugawaji wa nafasi za mawaziri.

Bwana Shearer ameongeza kwamba serikali mpya inaweza kusababisha mabadiliko chanya, na watu wakimbizi wa ndani na wakimbizi kuwa na uwezo wa kurejea nyumbani. 

Tayari karibu watu 800,000, kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM, wamerejea tangu kutiwa saini kwa makubaliano ya amani ya 2018.

Halikadhalika amesema, "taarifa ya kwanza ya pamoja kutoka kwa mamlaka mpya, yaani Rais na Makamu wa Rais, iliwasihi watu kutoka vituo vya ulinzi wa raia na nchi jirani warudi majumbani kwao. Ujumbe wao wa pamoja ni muhimu na kwa wakati unaofaa, kabla ya msimu wa mvua na pia msimu wa upanzi. Ujumbe huo, kwa kweli, unaiweka serikali mpya kuhakikisha kwamba maeneo wanakorejea ni salama."

Kwa upande wake, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNMISS umeongeza uwepo wake wa ulinzi ili kuimarisha imani katika maeneo wanakorejea wakimbizi. Hatahivyo, mwakilishi maalum huyo amesema ukosefu wa huduma za msingi za kiafya na elimu katika maeneo ya vijijini kumekatisha tamaa wengi waliotaka kurudi.

Bwana Shearer ambaye pia ni mkuu wa UNMISS amesema serikali mpya inakabiliwa na changamoto katika siku za awali ambazo zinajaribu umoja wake, hususan hitaji la kuendelea kwenye mpangilio wa usalama ambapo utekelezaji wake unasuasua. Aidha serikali mpya pia inakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu katika majimbo mengi, haswakutokana na mafuriko makubwa ya mwaka jana ambayo yaliharibu mazao, kuchafua maji, na kusababisha kupoteza mifugo.

Mwakilishi huyo Maalum amesema jamii ya kimataifa inaweza kuegemea upande wa tahadhari ili kutorudia makosa yaliyopita, ambayo amesema ni sawa, lakini akaongeza kuwa haiwezi kurudi nyuma kungoja kuona kile kitakachotokea kabla ya kuweka dhamira yake, "vitendo vyetu vinaweza kushinikiza Sudani Kusini kuelekea amani endelevu au kutokufanya kwetu kunaweza kutofaulu.

Mwakilishi wa kudumu wa Sudan Kusini kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Akuei Bona Malwal alilishukuru Baraza la Usalama kwa msaada wake kwa nchi yake. 

Amesema wakati wanachama wengi wa Baraza hilo walitaja matunda ya amani nchini Sudan Kusini, serikali ya mpito haipaswi kuanza jukumu lake jipya na vikwazo kama njia ya kusonga mbele.

Ameongeza kuwa, "serikali hii itakuwa serikali mpya, na nadhani jamii ya kimataifa inapaswa kuwa katika nafasi ya kuwapa fursa ili waweze kusongesha mbele watu wa Sudani Kusini. Lakini ikiwa utawafunga na vikwazo, ninahofia mafanikio yao yatadidimizwa. Lakini uamuzi ni wenu. "

 Balozi Malwal ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kutoa msaada unaohitajika sana na msaada kwa watu wa Sudani Kusini ili makubaliano ya amani yawe endelevu. Ameongeza kuwa serikali ijayo itahitaji utaalam wa kiufundi, vifaa na utaalamu maalumu ili kuanzisha maeneo ambayo yanakalika kwa ajili ya kurejea kwa amni wakimbizi wa ndani na wakimbizi kutoka nchi jirani.

Balozi huyo amesema, "ombi letu kwa wanachama wapenda amani wa jamii ya kimataida ni hili, iwapo ulisimama na watu wa Sudan Kuisni wakati wa kipindi kigumu cha miaka sita, huu ni muda muafaka wa kuimarisha msaada maradufu au mara tatu kwa ajili ya watu wa Sudan Kusini kwa ajili ya amani ya kuhudumu na umoja Sudan Kusini."