Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Naona nuru Koch, Sudan Kusini nina hakika hatutakimbia tena na watoto wetu- Bi. Nyakuaikoch

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini Sudan Kusini, David Shearer alipotembelea soko eneo la Koch, jimboni Unity State nchini Sudan Kusini
UNMISS\Nektarios Markogiannis
Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini Sudan Kusini, David Shearer alipotembelea soko eneo la Koch, jimboni Unity State nchini Sudan Kusini

Naona nuru Koch, Sudan Kusini nina hakika hatutakimbia tena na watoto wetu- Bi. Nyakuaikoch

Amani na Usalama

Mfuko mpya wa udhamini ulioanzishwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS pamoja na wahisaji unaleta  matumaini mapya kwa wakazi wa kaunti ya Koch jimboni Unity nchini humo. 

Eneo la Koch jimboni Unity nchini Sudan Kusini watoto wakiimba kwa furaha na matumaini, wakati wa ujio wa Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini David Shearer, kwenye eneo hili ambalo vita vya miaka mitano vilisambaratisha wengi kama asemavyo mkazi wa hapa Mary Nyakuaikochi.

Bi. Nyakuaikoch amesema, “baadhi ya watu walikimbia ili kuokoa maisha yao. Walikimbia na watoto wao huku wakiacha mali zao. Waliporejea kila kitu kilikuwa kimeporwa.”

Mkataba mpya wa amani wa mwezi Septemba mwaka jana umerejesha utulivu lakini ingawa watu wanarejea, bado hakuna mbinu za kuwawezesha kupata kipato, sokoni bado vibanda ni vichache, hospitali nayo haina vifaa vya kutosha na shule ya sekondari bado imefungwa.

Baada ya kutembelea soko, kukagua hospitali na kuzungumza na viongozi wa , Bwana Shearer amesema,“ni eneo masikini sana na ndio sababu ya mzozo hapa. Watu wengi wamekimbia makazi yao na kuhamia kituo chetu cha kuhifadhi wakimbizi. Iwapo tunaweza kurejesha huduma hapa na kuanza kuendeleza hili eneo basi tutakuwa na uhakika kuwa watu wataondoka kituoni na kuhamia hapa. Kwa hiyo moja ya mradi tunaotaka kufanya hapa kupitia mfuko wa udhamini ni ujenzi wa shule ya seondari.Watu hapa wanathamini elimu lakini shule za sekondari ni chache. Kwa hiyo kwa kujenga shule hapa tutaimarisha maridhiano na kupunguza mzozo kwa sababu watu watajikita kuhakikisha watoto wao wanakwenda shuleni.”

UNMISS inasema kuwa mfuko huo pia utasaidia kukarabati hospitali, kujenga mahakama, kusaidia manusura wa ukatili wa kingono na kijinsia, kukarabati masoko na barabara na kusaidia wanawake kuanzisha biashara. Walinda amani kwa upande wao watazuia ghasia huku mihadhara ya amani itasaidia kuleta jamii pamoja.

Wakati Bwana Shearer akisema kuwa hisia zake ni kwamba wakazi wa Koch hawataki tena vita na viongozi wa Sudan Kusini wahakikishe wanasaka suluhu kwa njia ya kidemokrasia na maridhiano na si kwa kupigana, Bi. Mary Nyakuaikoch, anasema,  “nina furaha kuwa amani itapatikana. Wanawake hawatakuwa wanakimbia tena wakiwa wamebeba watoto wao na kuugua wakiwa porini. Wana huduma bora za matibabu, wana shule ambako watoto wao watakwenda na huduma nyingi zaidi zinakuja kwenye jamii.”

Mfuko huo wa udhamiti wa maridhiano, utulivu na mnepo utatumia jumla ya dola milioni 5.2 kwa kipindi cha miaka miwili kutekeleza miradi mbalimbali itakayoongozwa na shirika la World Relief na muungaon wa mashirika ya kiraia yakiwemo CARE, Baraza la Wakimbizi la Denmark na Mercy Corps.