Watu milioni 45 wanakabiliwa na janga la njaa kusini mwa Afrika:WFP

16 Januari 2020

Watu milioni 45 wengi wakiwa wanawake na watoto katika mataifa 16 ya nchi zinazoendelea Kusini mwa Afrika wanakabiliwa na hali mbaya ya kutokuwa na uhakika wa chakula kufuatia kujirudia kwa hali ya ukame, kusambaa kwa mafuriko na kuyumba kwa uchumi.

Kwa mujibu wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP wakati hali ikizidi kuwa mbaya katika mataifa hayo dunia inapaswa kuchukua hatua kuingia sasa ili kuokoa Maisha na kuziwezesha jamii kuwa na mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Mkurugenzi wa WFP kanda ya Kusini mwa Afrika Lola Castro amesema “Janga la njaa liko katika kiwango ambacho hatujawahi kukishuhudia hapo nyuma na Ushahidi unaonyesha kwamba hali itakuwa mbaya zaidi. Msimu wa kila mwaka wa vimbunga umeanza na hatuwezi kumudu marudio ya uharibifu mkubwa uliosababishwa na vimbunga visivyo vya kawaida mwaka jana.”

Ameongeza kwamba wakati kipaumbele kwa sasa ni mamilioni ya watu wanaohitaji msaada wa haraka , kuwajengea mnepo mamilioni wengine walio katika tishio kubwa la ongezeko la athari za ukame na vimbunga ni suala muhimu sana.

Bi. Castro amesema “Msimu wa muambo unazidi kushika kasi wakati huu wa kuelekea mavuno Aprili na Mei, hivyo jumuiya ya kimataifa lazima iongeze haraka msaada wa dharura kwa mamilioni ya waliop na njaa Kusini mwa Afrika na pia uwekezaji wa muda mrefu kuwawezesha watu wa ukanda huo kuwa na mnepo wa kukabili athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi.

WFP inapanga kutoa msaada wa msimu wa muambo kwa watu milioni 8.3 katika nchi nane walio katika hali mbaya ya dharura njaa ambazo ni Zimbabwe, Zambia, Msumbiji, Madagascar, Namibia, Lesotho, Eswatini na Malawi.

Hadi kufikia sasa WFP imepata dola milioni 205 tu kati ya dola milioni 489 inazohitaji kuwasaidia watu hao na hivyo kulazimika kukopa ili kuhakikisha chakula kinawafikia wenye mahitaji.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud