Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kurejeshwa kwa doria ya MINUSCA Bangui kwakaribishwa kwa mikono miwili na wakazi

Mlinda amani akiwa doria katika mtaa wa PK5 Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati,CAR.
MINUSCA Photo
Mlinda amani akiwa doria katika mtaa wa PK5 Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati,CAR.

Kurejeshwa kwa doria ya MINUSCA Bangui kwakaribishwa kwa mikono miwili na wakazi

Amani na Usalama

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR, ujulikanao kama MINUSCA umerejesha shughuli za kushika doria katika mjii mkuu Bangui au PK5

Hatua hiyo imekuja kufuatia ombi la jamii baada ya mgogoro wakati wa kipindi cha Krismasi kati ya wafanyabiashara na vikundi vya watu waliojihami ambao hushikilia mji huo ambako watu zaidi ya 30 walipoteza Maisha katika vurugu hizo za krismasi. Kanali Andjia Christian Axel, ni mkurugenzi mkuu wa operesheni katika wizara ya usalama wa ndani.

(Sauti ya Andjia)

“Baada ya matukio ya hivi majuzi, na kufuatia ombi la raia mkutano wa uratibu ulifanyika MINUSCA. Pamoja na rais wa kamati ya kukabiliana na majanga, MINUSCA, na wizara ya usalama wa ndani, tumeweka utaratibu na muongozo kuhusu kurejea kwa vikosi vya usalama katika wilaya za ndani ya mji wa Bangui.”

Tangu kurudi kwa vikosi vya MINUSCA hali ya utulivu imerejea na ujumbe huo unahakikisha uwepo wa kikosi chake cha polisi kwa ajili ya kuondoa hofu miongoni mwa wakazi na uungwaji mkono na jamii.Ali Hassan Kahin ni mratibu wa polisi wa jamii  mjini Bangui

(Sauti ya Ali)

“Leo asubuhi tulienda kufanya doria kwa gari baadaye kwa mguu. Polisi walizungumza na jamii ambao walitoa shukrani zao. Mkurugenzi Mkuu wa operesheni alielekeza vikosi mashinani, aliweka juhudi zote. Anakuwepo kabla ya kuanza kwa operesheni yeyote kuzungumza na watu, Sisi pia tunaingilia kati kukumbusha wakazi kuhusu uwepo wetu ambao wanauhitaji.”

Kwa wakazi hali ni ile ya mgeni njoo mwenyeji apone. Marthe Songbet ni mkazi wa Bangui

(Sauti ya Marthe)

"Ilikuwa ni picha nzuri kuona MINUSCA, polisi na vikosi vya usalama. Hii ni moja ya aina za hatua tunazozitaka katika nchi hii.”

Serikali kwa kushirikiana na MINUSCA na wadau wamejizatiti kupokonya silaha mtu yeyote aliye na silaha katika eneo la Bangui pia kuchukua na kushikilia maeneo ambayo yanatawaliwa na makundi yaliyojihami ambayo yanawanyanyasa raia katika wilaya hiyo.