Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sitisheni uhasama, dunia inashuhudia migogoro zaidi katika karne hii-Antonio Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres akizunugmza na waandishi wa habari makao makuu ya Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Mark Garten)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres akizunugmza na waandishi wa habari makao makuu ya Umoja wa Mataifa.

Sitisheni uhasama, dunia inashuhudia migogoro zaidi katika karne hii-Antonio Guterres

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres leo Jumatatu amesema migogoro ya mataifa inachangia katika nchi nyingi zaidi kuchukua uamuzi ambao matokeo yake hayatabiriki na yanazua hatari kubwa ya matokeo ya mipango mibovu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani, Guterres amesema, “mwaka huu mpya umeanza na dunia iliyo na mtikisiko. Tunaishi katika zama hatari. Migogoro ya mataifa iko katika viwango vya juu zaidi katika karne hii, na misukosuko hii inapanda. Hata mkataba wa udhibiti wa silaha za nyuklia haupaswi kupuuzwa.”

Bwana Guterres ameongeza kwamba, biashara na mizozo ya kiteknolojia inaathiri masoko ya ulimwengu, inakwamisha ukuaji na kupanua ukosefu wa usawa.

Katibu Mkuu huyo amesema wakati hayo yakifanyika, “dunia yetu inateketea, janga la mabadiliko ya tabianchi linaongezeka. Katika sehemu mbali mbali za ulimwengu tunashuhudia watu waliofadhaika na walio na hasira. Tunashuhudia ukosefu wa utulivu katika jamii na kuenea kwa misimamo mikali na utaifa na ongezeko la ugaidi hususan bara la Afrika.”

Guteress amesema hali hiyo haipaswi kuendelea.

Katibu Mkuu Guterres amehitimisha kwa ujumbe kwa viongozi wa dunia akisema, “(ujumbe wangu), unaeleweka na ni wazi. Sitisheni uhasama. Watu wajizuie. Mazungumzo yaanze upya. Anzeni upya ushirikiano kimataifa. Hebu tusisahau madhila yatokanayo na vita. Kama kawaida watu wa kawaida ndio hulipa gharama kubwa. Ni jukumu letu sote kuepusha hilo.”