Athari za nyuklia hazina mipaka, kuziangamiza silaha hizo ni lazima: Guterres.
Histori ya majaribio ya nyuklia ni ya machungu na ambayo imeathiri watu zaidi ya 2,000 wengi wao kutoka katika jamii za wanyonge zisizojiweza duniani. Hiyo ni kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, katika ujumbe wake maalumu hii leo wa siku ya kimataifa ya kupinga majaribio ya nyuklia. Athari hizo mbaya zisizojali mipaka ya kimataifa ni dhahiri pia katika mazingira, afya, uhakika wa chakula na maendeleo ya kiuchumi.
Guterres ameongeza kuwa tangu kumalizika kwa vita baridi , kumekuwa na desturi ya kupinga majaribio ya silaha za nyuklia ambayo imekiukwa na taifa moja tu katika karne hii.
Siku ya kimataifa ya kupinga majaribio ya silaha za nyuklia ilianza kuadhimishwa baada ya kupitishwa azimio na Baraza Kuu Disemba 2 mwaka 2009 lililotaka kuongeza uchagizaji dhidi ya athari za majaribio ya silaha za nyuklia na haja ya kukomesha majaribio hayo kama njia ya kuwa na dunia isiyo na silaha za nyuklia. Azimio hiloliliwasilishwa na Kazakhstan na kuungwa mkono na mataifa mengine.
Mwakilishi wa kudumu wa Kazakhstani katika Umoja wa Mataifa ni Kairat Umarovakizungumza na UN News amefafanua kuhusu athari za majaribio ya silaha hizo.
“Madhara ya majaribio ya Nyuklia angani, ardhini na chini ya ardhi ni makubwa, nisawa na kunyunyuzia kilo 300 za chembechembe zenye sumu za madini ya plotonium katika eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba elf 18, eneo kubwa ambalo leo hii halitumiki tena”
Ameongeza kuwa watu wengi katika mameneo ambayo kumefanyika majaribio hayo hawataki kuzaa kwa hofu ya kupata watoto walio na ulemavu kama kutokuwa na mikono wala miguu kutokana na sumu ya athari za nyuklia.
Siku hii ya kimataifa pia ni siku ya kukumbuka kufungwa kwa kituo cha majaribio ya nyuklia cha Urusi hapo Agosti 29 mwaka 1991 kilichokuwa sehemu ya Semipalatinsk.
Kituo hicho japo kilimilikiwa na Urusi lakini kilikuwa nchini Kazakhstan, ambapo zamani eneo lote hilo lilikuwa chini ya muungano wa Soviet kabla ya kusambaratika.