Kinara wa UN azindua ajenda yake ya kudhibiti silaha duniani

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametangaza mwelekeo wake mpya kuhusu udhibiti wa silaha katika juhudi za kutokomeza silaha za nyuklia pamoja na silaha zingine zinazoweza kusababisha maangamizi dunia kutokana na makosa iwe ya kiufundi, kielektroniki au ya kibinadamu.
Antonio Guterres akizindua ajenda yake hiyo wakati akihutubia kwenye Chuo Kikuu cha Geneva, huko Uswisi, amesema, “Umoja wa Mataifa uliundwa kwa lengo la kuondoa vita itumikayo kama chombo cha sera ya kigeni. Lakini miongo saba imepita, dunia yetu bado ni hatari zaidi na ilivyokuwa kabla,” ameonya.
Bw Guterres amefafanua, “udhibiti wa silaha unazuia na kukomesha vita. Udhibiti pia unaunga mkono maendeleo endelevu. Na udhibiti ndio jibu kwa misingi yetu.”
Amesema uzinduzi huo wa ajenda mpya aliyopatia jina kutunza mustakabali wetu wote, umekuja kwa wakati akisema udhibiti wa silaha umekuwa kama wimbo wa kila siku, wakati mwingine kuhusu Iran na Syria , na siku nyingine kuhusu rasi ya Korea.
Ajenda hiyo inalenga vipaumbele vitatu- silaha za maangamizi, silaha za kawaida na teknolojia mpya kuhusu vita.
Bwana Guterres amesisitiza kuwa, udhibiti wa silaha za nyuklia, na silaha za kemikali na za kibayolojia unaweza kuokoa binadamu akibaini kuwa bado silaha takriban 15,000 za nyuklia zimehifadhiwa sehemu mbalimbali duniani na ziko tayari kutumiwa wakati wowote ule.
Amesema kuwa mataifa yaliyo na silaha za nyuklia yana wajibu wa kwanza wa kuwezesha dunia kuepukana na janga.
Katika mantiki hiyo ameziomba Marekani na Urusi kuondoa tofauti zao ili zitafute suluhu ya mgogoro kuhusu mkataba wa makombora ya masafa ya kati yenye uwezo wa kubeba silaha za nyuklia.
Ameziomba pia kurefusha mkataba mpya wa kuzidi kupunguza silaha nzito ambao pia unahusu silaha za kinga kwa kifupi START, ambao unakaribia kumalizika katika kipindi cha miaka mitatu kutoka sasa.
Pia amezitaka zichukuwe hatua mpya za kupunguza mrundikano wa silaha za nyuklia.
Udhibiti wa silaha utaokoa maisha na zaidi ya yote utaokoa raia wa kawaida ambao wanaendelea kuteseka kutokana na migogoro ya kivita.
Ameongeza kuwa mbali na watu wengi kuuawa na kujeruhiwa, migogoro inasababisha watu wengi kuacha nyumba zao, wakati mwingine kukosa chakula, huduma za kiafya, elimu pamoja na mbinu za kuendeleza maisha yao.
Ametoa mifano kadhaa akisema kuwa hadi mwisho wa mwaka 2016 zaidi ya watu milioni 65 walihama makazi yao kutokana na migogoro ya kivita, ghasia na mateso.
“Juhudi zangu zitakuwa zinaegemea mno ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu, ambayo ndio msingi wa dunia yenye amani, maendeleo na afya bora,” amesema Guterres .
Katibu Mkuu amegusia pia bajeti zinazotumika kwenye masuala ya kijeshi akisema kuwa pamoja na ununuzi kuna ubadhilifu katika ununuzi wa silaha akisema unakausha hazina ambazo zingetumiwa kuinua miradi ya maendeleo endelevu.
Amesema mwaka jana pekee dola zaidi ya trilioni 1.7 zilitumiwa kwenye manunuzi ya silaha, kiwango ambacho amesema ni kikubwa sana kuwahi kufikiwa tangu kuangushwa kwa ukuta wa Berlin nchini Ujerumani.
Kwa mujibu wa Guterres, kiwango hicho ni mara 80 zaidi ya pesa zinazohitajika katika misaada ya kibinadamu duniani kote.