Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya kutelekezwa kutokana na vita sasa mashamba ya Yathreb Iraq yashamiri tena:UNHCR

Mitaa ya mji wa Baghdad, Iraq kabla ya kuibuka kwa machafuko
UNAMI
Mitaa ya mji wa Baghdad, Iraq kabla ya kuibuka kwa machafuko

Baada ya kutelekezwa kutokana na vita sasa mashamba ya Yathreb Iraq yashamiri tena:UNHCR

Amani na Usalama

Mamia ya raia wa Iraq waliokimbia machafuko na vita kwenye mji wa Yathreb jimboni Salahudine wameanza kurejea nyumbani na kufufua matumaini ya maisha na kilimo walichokitelekeza kwa muda mrefu. 

Kijijini Yathreb rangi ya kijani imetanda mashambani katika kijiji hiki ambacho awali kikijulikana na kapu la matunda la Iraq kutokana na kuzalisha matunda mengi na mbogamboga nchini humo kama vile zabibu, matikiti, mapichi na mboga za majani zikiwemo bamia anazolima Matra Nsayefu mmoja wa wakimbizi waliorejea na anakumbuka siku aliyofungasha virago na kukimbia,“ulikuwa usiku mgumu sana wapiganaji walikuwa wakituvurumishia maroketi”

Mwaka 2014 watu wengi walikimbia Kijiji hiki wakihofia wapiganaji wa ISIS na walikimbilia sehemu mbalimbali za Iraq, wakasuburi huko kwa muda hadi sasa ambapo wameweza kurejea tena majumbani kwao na kwenye mashamba yao kama mkulima wa makomamanga Kutaiba Falal, “ndio nilikuwa naogopa kurejea , hali ilikuwa mbaya na hofu haikukwepeka. Na niliporejea niliumia sana kushuhudia hali halisi ya shamba langu.”

Mwaka 2016 zaidi ya asilimia 80 ya watu walirejea na kukuta nyumba zilizoteketezwa kwa moto, mashamba yaliyotelekezwa na mengine kuharibiwa vibaya kama anavyothibitisha Matra japo yeye alifurahi amerejea nyumbani,“nyumba yetu iliteketezwa kwa moto, kila kitu kiliungua, lakini tumepata makazi mengine hapa. Nilifurahi sana saana kurejea”

Kwa msaada wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR ,mfereji wa maji katika kijiji hicho ulisafishwa na kukarabatiwa na mifumo ya umwagiliaji ikawekwa na pia madaraja mengi na barabara zimekarabatiwa na kuanza kutumika tena. Lengo la UNHCR kufanya yote hayo ni kuzisaidia jamii kurejea nyumbani na kuanza upya maisha yao.