Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano Syria yasababisha mamia ya watu kukimbilia Iraq

Wakimbizi kutoka Syria wakiwa kambi ya Bardarash nchini Iraq.
© UNHCR/Rasheed Hussein Rasheed
Wakimbizi kutoka Syria wakiwa kambi ya Bardarash nchini Iraq.

Mapigano Syria yasababisha mamia ya watu kukimbilia Iraq

Wahamiaji na Wakimbizi

Wakimbizi kutoka Syria wameanza kuwasili katika kambi ya Bardarash iliyoko jimbo la Duhok kaskazini mwa Iraq kufuatia mashambulizi yanayoendelea kaskazini-mashariki mwa Iraq wakati huu ambapo mashirika ya Umoja wa Mataifa yameripoti vifo pande zote kutokana na mapigano hayo.

Kambini Bardarash jimboni Duhok nchini IRaq, wakimbizi kutoka Syria tayari wamewasili na wanapata mlo , wengine wakiwa hoi  kutokana na uchovu wa safari.

Takriban wakimbizi 1,000 kutoka Syria wamewasili eneo la Kurdish nchini Iraq Said Abdul Ahmad ni mmoja wao.

(Sauti ya Said)

“Nashukuru Mungu tuliondoka, tumekuja hapa kwa msaada wa Mungu na msaada wenu, safari ilikuwa ngumu, barabara ilijaa milima, uoga ulitufanya kuja hapa, tunashukuru Mungu wakati tuliwasili hapa, tulijisikia nafuu, tunamshukuru Mungu.”

Watu 278 walisafirishwa kwa basi hadi kambi ya Bardarash mapema wiki hii kutoka maeneo ya mpakani huku wengine 570 wakiwa kituo cha mapokezi katika kambi ya Domiz. 

Rizqan Mahmoud Hassan, ni mkimbizi kutoka Qameshly

(Sauti ya Hassan)

“Nina umri wa miaka 35. Tumekuwa barabarani kwa siku mbili. Tulikimbia kwa sababu ya mabomu na mashambulizi ya angani huko Qamishli kwa sababu watu walikuwa wakiuwawa au kujeruhiwa.”

Wakimbizi wanaohifadhiwa katika kambi hiyo inayosimamiwa na UNHCR wanasema wametoka maeneo ya Terbasiye, Hassakah na Qamishly ambako tangu tarehe 9 mwezi huu wa Oktoba kumekuwepo na mashambulizi kila uchao.