Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bado tuna wasiwasi mkubwa wa usalama wa watu milioni 3 Syria:UN

Watoto walioyakimbia mapigano mjini Idlib Syria
©UNICEF/Watad
Watoto walioyakimbia mapigano mjini Idlib Syria

Bado tuna wasiwasi mkubwa wa usalama wa watu milioni 3 Syria:UN

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umesema bado unawasiwasi mkubwa wa hatma ya usalama wa takriban raia milioni 3 huko Idlib Syria ambako zaidi ya nusu ya watu wote wametawanywa na kuwa wakimbizi wa ndani kufuatia ripoti za kuendelea kwa mashambulizi ya anga katika eneo hilo.

Kupitia taarifa iliyosomwa na msemaji wa Umoja wa Mataifa mbele ya waandishi wa Habari hii leo mjini New York Marekani Stephane Dijarric “Jumamosi mwishoni mwa wiki Umoja wa Mataifa ulifanikiwa kuwepo kwa usitishaji wa mashambulizi kwa saa sita ambazo ziliruhusu zaidi ya watu 250,000 kukimbia kwa usalama.”

Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa unaendelea na juhudi za kuzishawishi pande zote kuruhusu raia wanaotaka kuondoka katika maeneo yaliyoathirika, kuondoka kwa usalama.

Umoja wa Mataifa unasema “Katika siku tatu zilizopita jamii 39 zimeripotiwa kuathirika na uvurumishwaji wa makombora katika majimbo ya Kaskazini mwa Harma, Kusini mwa Idlib na Magharibi mwa Aleppo huku jamii 47 zikiripotiwa kupigwa na mashambulizi ya anga  .”

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa idadi mpya ya watu waliotawanywa na machafuko yanayoendelea Syria tangu mwishoni mwa mwezi aprili sasa imefikia zaidi ya laki nne , wanawake, watoto na wanaume, na wengi wao wametawanywa mara kadhaa.

Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa pande zote kuhakikisha ulinzi wa raia na kuruhusu bila vikwazo au mashariti wahudumu wote wa misaada ya kibinadamu ili kutoa msaada wa kibinadamu wa kuokoa maisha kwa wote wanaouhitaji.