Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahanga wa mashambulizi ya anga Syria wanafumbiwa macho-Bachelet

Familia nchini Syria ikisafiri kwa lori ikikimbia eneo la mapigano karibu na Kafr Lusein mweiz Mei 2019
© UNICEF/Ahmad Al Ahmad
Familia nchini Syria ikisafiri kwa lori ikikimbia eneo la mapigano karibu na Kafr Lusein mweiz Mei 2019

Wahanga wa mashambulizi ya anga Syria wanafumbiwa macho-Bachelet

Amani na Usalama

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amemulika hali ya kitendo cha jumuiya ya kimataifa kupuuza ongezeko la vifo vya raia kutokana na mashambulizi ya anga katika maeneo ya Idlib na maeneo mengine kaskazini magharibi mwa Syria. 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi, msemaji wa Kamishna Mkuu, Ruppert Colville amemnukuu Bi. Bachelet akisema,‘licha ya wito mbali mbali wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuheshimu masharti ya kujizuia na kutofautisha katika kuendesha uhasama, mashambulizi ya anga hivi karibuni kwa serikali na wafuasi wao yameendelea kulenga vituo vya afya, shule na miundombinu mingine ya raia ikiwemo masoko na maduka ya mikate.”

Bi. Bachelet ameongeza kwamba haya ni maeneo ya raia na kwa mwelekeo na matukio ya mashambulizi hayo inaonekana kwamba sio matukio ya kimakosa. Aidha taarifa ya Kamishna Mkuu imemnukuu akisema, “mashambulizi ya kulenga dhidi ya raia ni vita vya uhalifu na wanaotekeleza au kutoa amri yatekelezwe wanawajibika kisheria kwa vitendo vyao.”

Licha ya mashambulizi ya mara kwa mara kwa mamamia ya maelfu ya watoto na wanawake kuuwawa Syria tangu mwaka 2011 na licha ya kwamba sasa hizi idadi ni kubwa kiasi cha kutojulikana lakini hili halizungumiziwi katika anga za kimataifa ikilinganishwa na awali wakati waathiriwa walikuwa katika makumi, mamia na hata maelfu.

Bwana Colville amemnukuu Bi. Bachelet akisema, “kwa sasa, mashambulizi ya anga huua na kulemaza idadi kubwa ya raia mara kadhaa kwa wiki na majibu yake ni kupuuza kwa pamoja huku baraza la usalama likikosa nguvu kufuatia kutokubaliana kwa wajumbe wake watano wa kudumu kuhusu matumizi yao ya mamlaka na ushawishi kutokomeza mapigano na mauji mara moja.”

Ofisi ya haki za binadamu kwa sasa imeandikisha vifo vya takriban raia 450, ikiwemo 91 ambao waliuuawa na mashambulizi ya anga katika kipindi cha siku kumi tangu kampeni ya mwisho ya serikali na wafuasi wake kaskazini magharibi mwa Syria yalipoanza takriban miaka miezi mitatu iliyopita.

Bi. Bachelet, ameongeza kwamba licha ya kuwa sehemu ya makubaliano ya kusitisha uhasama ya mwaka 2017 na makubaliano ya 2018 ya kupunguza vitendo vya kijeshi, Idlib na viunga vyake vinaendelea kushuhudia ongezeko la vitendo vya kijeshi huku hali ya haki za kibinadamu na msaada wa kibinadamu ikiwa mbaya kwa mamiloni ya raia wanaoishi huko.

Kwa mantiki hiyo, kamishna mkuu huyo ametoa wito kwa pande zenye ushawisi ikiwemo zilizokubali kupunugza uhasama kama sehemu ya makubaliano ya kupunguza uhasama wanapaswa kutumia ushawishi wao kutokomeza kampenzi za sasa hizi za kijeshi na kuleta pande kinzani kwenye meza ya mazungumzo kama kiungo muhimu ili kutoa fursa ya kufanikisha majadiliano ya kisiasa yanayoendelea.