Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde pande kinzani Syria zingatieni haki za raia- Bachelet

Watoto wakiwa katika hema wanalolitumia kama darasa katika kambi ya wakimbizi ya Junaina kaskazini mwa Idlib, Syria.
UNICEF/UN0248439/Watad
Watoto wakiwa katika hema wanalolitumia kama darasa katika kambi ya wakimbizi ya Junaina kaskazini mwa Idlib, Syria.

Chonde chonde pande kinzani Syria zingatieni haki za raia- Bachelet

Amani na Usalama

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet amesihi pande kinzani kwenye mzozo nchini Syria ziheshimu sheria za kimataifa pindi zinapoendesha operesheni zao za kijeshi wakati huu ambapo usalama wa raia huko Idlib unazidi kuzorota. 

Bi. Bachelet amepaza sauti hiyo wakati huu ambapo imeripotiwa kuongezeka kwa mashambulio huko Idlib nchini Syria ambayo yanafanywa na vikosi vya serikali na washirika wao sambamba na vikundi vilivyojihami.

Yaelezwa kuwa mashambulio hayo yaliyoanza mwezi Disemba mwaka jana yamesababisha vifo vya raia huku maelfu wakikimbia makazi yao, jambo linalozidi kumtia wasiwasi mkubwa Kamishna Mkuu Bachelet.

Msemaji wa ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Rupert Colville akizungumza na waandishi wa habari  hii leo mjini Geneva, Uswisi amemnukuu Bi. Bachelet akisema kuwa mashambulizi hayo kwenye maeneo yasiyopaswa kuwa na shughuli za kijeshi kama vile Idlib na jimbo la Hama na Allepo yamezidi kushamiri.

(Sauti ya Rupert Colville)

“Na jana kulikuwepo na tukio baya zaidi ambapo raia 16 wakiwemo wanawake na watoto waliuawa na wengine zaidi ya 70 walijeruhiwa kwenye viunga vya Kosur vya Idlib. Mashambulizi yalifanywa kwa kutumia vilipuzi viwili, ambapo kilipuzi cha pili kinaonekana kilitengenezwa kuua au kulemaza watu wakiwemo wahudumu wa afya wanaojaribu kusaidia majeruhi wa shambulio la kwanza. Kwa hiyo mashambulio mawili.”

Hofu zaidi ya Bi. Bachelet ni hali  ya familia 200 wakiwemo wanawake na watoto ambao yaripotiwa wamenasa kwenye eneo lililo chini ya magaidi wa ISIL na wanazuia kuondoka kwenye eneo hilo lililogubikwana makombora ya angani na mashambulizi ya ardhini.

Kamishna Mkuu amesihi pande husika kwenye mzozo huo ulioanza mwaka 2011 wazingatie kanuni za kimataifa.