Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Somalia iko katika wakati muhimu mshikamano wahitajika kwa ajili ya mustakbali wa amani:Swan 

Raia wa Somalia wakiwa wamesimama nje ya kioski eneo la soko katika bandari ya Kismayo, Kusini mwa Somalia.
UN Photo/Stuart Price
Raia wa Somalia wakiwa wamesimama nje ya kioski eneo la soko katika bandari ya Kismayo, Kusini mwa Somalia.

Somalia iko katika wakati muhimu mshikamano wahitajika kwa ajili ya mustakbali wa amani:Swan 

Amani na Usalama

Somalia ikielekea wakati muhimu katika mustakabali wa amani ya taifa hilo lililokuwa kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa zaidi ya miongo mwili sasa, imeaswa na Umoja wa Mataifa kuonyesha mshikamano katika malengo iliyojiwekea 2020. 

Jiji la Kismayo kama yalivyo maeneo mengine ya Somalia vita vya zaidi ya miaka 20 vimepoteza maisha ya maelfu ya watu na matumaini ya kuwa na amani na maendeleo, lakini sasa hali inabadilika kutokana na jitihada za Umoja wa Mataifa na wadau wengine wa kikanda ambao wanafunga safari kila uchao kwenda kila jimbo la nchi hiyo ya pembe ya Afrika kuhakikisha ajenda inaeleweka na mshikamano unatolewa hasa kuelekea uchaguzi mkuu hapo mwakani.

Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia UNSOM na mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu bwana James Swan akiambatana na wadau wengine, wamezuru mji mkuu wa Jubaland , Kismayo na kukutana na viongozi ili kujadili jinsi gani ya kutekeleza vipaumbele hivyo vya taifa mwaka 2020

Tuko hapa kukutana na wadau mbalimbali na kusikia mtazamo wao kuhusu jinsi gani vipaumbele muhimu vya taifa vinaweza kutimizwa mwaka 2020. Hivi vinajumuisha maandalizi ya uchaguzi wa kura moja mtu mmoja, kukamilisha katiba ya shirikisho, kuendelea na mchakato wa kupunguza madeni na vita dhidi ya Al-Shabaab.”

Kwa niaba ya ujumbe aliokwenda nao James Swan amesema "Tukielekea katika mwaka huo muhimu , wawakilishi wa baadhi ya washirika mbalimbali wa Somalia wanawasiliana na mamlaka ya kitaifa , serikali za shirikisho, wazee, na asasi za kiraia nchi nzima. Tunasikitika kwamba katika ziara ya leo baadhi ya asasi za kiraia na viongozi wa kijamii walioalikwa wameshindwa kuja kukutana nasi”

Ujumbe uliowasili Kismayo umejumuisha balozi wa Muungano wa Ulaya Somalia, mkuu wa mpango wa Muungano wa Afrika (AU) nchini Somalia na afisa kutoka mamlaka ya muungano wa serikali kuhusu maendeleo IGAD. Ujumbe huo umekutana na Rais wa Jubaland Ahmed Mohamed Islam Madobe, viongozi wa kijamii, wawakilishi wa asasi za kiraia na viongozi wa upinzani.

Bwana Swan amewachagiza viongozi wote wa Somalia , taasisi na jamii kujihusisha katika majadiliano ili kuafiki njia bora ya kusonga mbele na kushirikiana katika kutimiza vipaumbele walivyokubalina kwa mwaka ujao.