Usalama wa Somalia bado ni wa wasiwasi, aonya Mkuu wa UNSOM

Usalama wa Somalia bado ni wa wasiwasi, aonya Mkuu wa UNSOM
Katika hotuba yake ya kwanza kwa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani hii leo, mwakilishi maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, James Swan ameeleza hatua ilizozipiga Somalia katika kuboresha mambo kikatiba na kiusalama, miongoni mwa vipengele vingine, lakini akaonya kuwa mwanya wa kufikia hatua muhimu zaidi unazidi kuwa finyu.
Bwana Swan amesema katika safari zake kuzunguka Somalia ameoona mifano mingi ya kurejea katika hali bora, maendeleo, usalama na taasisi za serikali zinazofanya kazi. Amesema maendeleo hay ani ushuhuda wa nia lakini pia ajenda ya viongozi wa Somalia ya ujenzi wa amani na nchini.
Hata hivyo Bwana Swan ameeleza kuwa mafanikio hayo yako katika hatari ya kutofikia muda uliokubaliwa na maendeleo zaidi yanaweza kuchekelewa bila uwepo wa mazungumzo mengine na ushirikiano miongoni mwa wadau.
Akigeukia Jubaland, Swan amesema Umoja wa Mataifa unaendelea kuhimiza mchakato wa pamoja, uliokubaliwa kuhusu uchaguzi, ampapo bila hivyo kuna hatari kubwa ya kukosekana kwa utulivu ikiwa kutatokea matokeo ya kugombewa. Amesema, “matokeo yoyote kesho huko Jubaland, nawasihi wadau waoneshe kujizuia, waachane na vurugu, na watatue malalamiko kupitia mazungumzo.”
Naye Francisco Caetano Jose Madeira ambaye ni Mkuu wa vikosi vya Muungano wa Afrika, AU, nchini Somalia AMISOM amesema AMISOM imefanya mikutano na serikali ya kuu, maafisa wa majimbo na wagombea katika Jubaland katika juhudi za kushughulikia masuala yaliyoibuliwa na pande husika. Amesema, “pamoja na kuchelewa, ni matumaini yetu kuwa pande zote zitafikia uchaguzi ambao ni jumuifu, wa haki na amani kuimarisha umoja wa watu wa Jubaland.”
Kwa upande wake, Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika kushgughulikia masuala ya unyanyasaji wa kingono katika migogoro, Pramila Patten amewaeleza wajumbe wa Baraza kuwa unyanyasaji wa kingono nchini Somalia unasalia kuwa suala muhimu linalopaswa kuangaziwa. Amesema kuwa wanawake wasiohesabika na wasichana wanaishi kwa hofiu ya unyanyasaji wa kingono akiongeza kuwa waathirika mara nyingi hawaonekani na hawafikiwi wakiwa hawana pa kuripoti uhalifu hu una hawana pa kugeukia.