Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yalaani vikali shambulio la kigaidi lililoua zaidi ya watu 70 Mogadishu

Magari  yaliyoharibika kufuatia mashambulio mawili ya kujilipua yaliyofanywa na Al Shabaab nchini Somalia na kusababisha vifo vya makumi kadhaa ya watu.
UN /Stuart Price
Magari yaliyoharibika kufuatia mashambulio mawili ya kujilipua yaliyofanywa na Al Shabaab nchini Somalia na kusababisha vifo vya makumi kadhaa ya watu.

UN yalaani vikali shambulio la kigaidi lililoua zaidi ya watu 70 Mogadishu

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umelaani vikali shambulio la kigaidi lililofanyika leo Jumamosi Desemba 28 mwaka 2019 mjini Mogadishu nchini Somalia.

Kupitia taarifa iliyotolewa na msemaji wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa pole na kutuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza maisha katika tukio hilo na kuwatakia majeruhi wote ahuweni ya haraka.

Amesisitiza kwamba wahusika wote wa ukatili na unyama huo ni lazima wafikishwe mbele ya sheria.

Kwa mujibu wa duru za habari takriban watu 79 wameuawa na wengine 149 wamejeruhiwa baada ya bomu lililotegwa kwenye gari kulipuka kwenye eneo lililokuwa na pilika na watu wengi nje kidogo ya mji mkuu Mogadishu saa za asubuhi za Somalia.

Msemaji wa serikali ya Somalia Ismael Mukhtar amenukuliwa na vyombo vya habari akisema gaidi aliendesha gari lake lililokuwa na mabomu hadi kwenye kituo cha zamani cha ukaguzi cha Afgoye ambacho ni makutano maarufu yanayounganisha sehemu ya Kusini mwa Somalia na mji mkuu Mogadishu.

Bwana Mukhtar ameongeza kuwa miongoni mwa waliokufa katika shambulio hilo lililotokea wakati wa harakati nyingi asubuhi ni wanafunzi wa chuo kikuu, raia na askari.

Hakuna kinachohalalisha ugaidi

Katibu Mkuu amerejea kusitiza ahadi ya Umoja wa Mataifa kusaidia watu na serikali ya Somalia katika mchakato wao wa kusaka amani ya kudumu na maendeleo.

Naye mwakilishi wa umoja wa Mataifa nchini Somalia na mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNSOM, Bwana James Swan kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema anaalani vikali shambulio hilo la kikatili na kigaidi dhidi ya raia wasio na hatia akisisitiza kwamba wote waliohusika wanapaswa kufikishwa mbele ya mkono wa sharia na kuwajibishwa.

Amesisitiza kuwa hakuna sababu yoyote inayohalalisha ugaidi wa aina yoyote, kwa njia yoyote na mahali popote.