Katika umri wangu wa miaka 70 sijashuhudia ukame wa kiwango hiki- Mwananchi Somalia
Akiwa amesimama mbele ya kibanda chake kwenye makazi ya wakimbizi ya Kulmiye wilayani Luuq nchini Somalia, Ahmad Hassan Yarrow anatazama kile kilichosalia katika mto Juba, ambao ulikuwa ndio tegemeo la uhai wa eneo lao. Mto umekauka. “Katika umri wangu wa miaka 70 sijawahi kushuhudia ukame kama huu, katika vipindi vyote vya ukame vilivyopita,” anasema Bwana Yarrow katika makala iliyochapishwa kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa usaidizi nchini Somalia, UNSOM.