Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto 9 huuawa au kulemazwa kila siku nchini Afghanistan

Mkunga katika kituo cha afya cha Sa-e-Hause kwenye kijiji cha Tajikhan nchini Afghanistan akizungumza na mama aliyembeba mwanae mwenye umri wa miezi 5.
World Bank/Graham Crouch
Mkunga katika kituo cha afya cha Sa-e-Hause kwenye kijiji cha Tajikhan nchini Afghanistan akizungumza na mama aliyembeba mwanae mwenye umri wa miezi 5.

Watoto 9 huuawa au kulemazwa kila siku nchini Afghanistan

Amani na Usalama

Vita vilivyodumu kwa miaka 40 sasa nchini Afghanistan vimekuwa na madhara makubwa kwa watoto ambapo kila siku husababisha watoto 9 kuuawa au kusalia na ulemavu, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto,  UNICEF.

Kupitia ripoti yake iliyotolewa hii leo katika miji mitatu, Kabul Afghanistan, New York, Marekani na Geneva, Uswisi na kupatiwa jina Kutunza matumaini nchini Afghanistan; Linda watoto katika mzozo hatari zaidi duniani, UNICEF inasema kuwa kiwango cha watoto 9 kuuawa au kulemazwa kila siku ni kwa mwaka huu pekee wa 2019.

Ripoti inasema kiwango hicho ni ongezeko kwa asilimia 11 ikilinganishwa na mwaka 2018 na sababu kuu ni kuongezeka kwa mashambulio ya kujilipua kwa mabomu na mapigano ya ardhini kati ya majeshi ya serikali na yale yanayopinga serikali.

 “Hata kwa viwango vya chini vya Afghanistan, mwaka 2019 umekuwa hatari zaidi kwa watoto,” amesema Henrietta Fore, Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF akiongeza kuwa, “watoto na familia zao na jamii wameumizwa sana na madhara ya vita hivyo kila siku. Watoto hao hao wanahaha kukua, kwenda shule, kujifunza stadi na kujenga mustakabali wao wenyewe. Tunaweza na tunapaswa kuchukua hatua zaidi kuimarisha uwezo wa kumudu maisha na hata ujasiri.”

Takribani watoto 6,500 wameuawa kati ya 2009 na 2018

UNICEF inasema kuwa kati ya mwaka 2009 hadi mwaka 2018, takribani watoto 6,500 waliuawa na wengine 15,000 walijeruhiwa na kufanya Afghanistan kuwa eneo baya zaidi la vita kwa mwaka 2018.

Shirika hilo linasema kuwa kando ya madhara hayo ya moja kwa moja ya vita kwa watoto, maisha ya watoto nayo yameparaganyika kutokana na majanga ya asili, umaskini, na ukosefu wa maendeleo.

Ili kukabiliana na utapiamlo uliokithiri miongoni mwa watoto, UNICEF inashirikiana na wadau na tayari wasambaza matibabu kwa watoto 277,000 wenye  unyafuzi. Hata hivyo mradi huo unahitaji fedha zaidi ili kufikia watoto wengine 300,000 wenye mahitaji.

Ni kwa mantiki hiyo UNICEF inatoa ombi la dola milioni 323 ili kusaidia operesheni zake nchini Afghanistan kwa mwaka 2020, ombi ambalo hadi sasa limetimizwa kwa asilimia 25 tu.

Madhara ya vita kwa watoto na vijana Afghanistan

  • Watoto milioni 3.8 wanahitaji msaada wa kibinadamu

  • Mtoto 1 wa kike kati ya 3 anaozwa kabla ya kutimiza umri wa miaka 18
  • Watoto milioni 3.8 wenye umri wa kwenda shuleni hawako shuleni
  • Watoto 600,000 wenye umri wa chini ya miaka 5 wana unyafuzi
  • Asilimia 30 ya watoto wanatumikishwa
  • Vijana 400,000 wanaingia soko la ajira kila mwaka lakini wengi hawana stadi za kuweza kupata ajili ili waweze kumudu maisha ya kujikimu.

Vijana nao wamo

Akizungumzia takwimu za vijana wa Afghanistan, Mwakilishi mkazi wa UNICEF nchini humo Aboubacar Kampo amesema kuwa vijana hao “wanapaswa kufahamu kuwa matarajio yao ya kupata ajira ni zaidi ya kujiunga na vikundi vilivyojihami, au kukimbia nchi yao ili kusaka bahati nje ya nchi. Wakipatiwa msaada sahihi, wanaweza kuanza kuondokana na mzunguko wa ghasia na ukosefu wa maendeleo na kujenga mustakabali bora kwa ajili yao na taifa lao.”

Hivi sasa UNICEF inashirikiana na mamlaka za Afghanistan ikiwemo jamii ili kushughulikia tamaduni zilizopitwa na wakati ikiwemo watoto wa kike kutolewa kafara, ukatili majumbani na ukatili wa kingono.

Ingawa hivyo UNICEF inataka pande kinzani kwenye mzozo kuwajibika kwa kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu na za haki za bindamu ambazo zinataka watoto walindwe na maeneo kama shule na hospitali yasilengwe wakati wa mapigano, sambamba na kuhakikisha kuwa watoa misaada wanapatiwa fursa ya kufanya hivyo.