Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rushwa yawa  hoja kuu wakati wa upigaji kura- Guterres

Bango lenye ujumbe wa ufisadi nchini Namibia
Bank ya Dunia/Philip Schuler
Bango lenye ujumbe wa ufisadi nchini Namibia

Rushwa yawa  hoja kuu wakati wa upigaji kura- Guterres

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Leo ni siku ya kimataifa ya kutokomeza rushwa ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anasema vitendo vya ufisadi vimeshamiri nchi zote iwe maskini au tajiri, iwe za kaskazini au kusini.
 

Katika ujumbe wake aliotoa leo wakati huu ambapo Umoja wa Mataifa unasema kuwa matrilioni ya dola sawa na zaidi ya asilimia tano la pato la ndani duniani huibwa au kulipwa kifisadi, Guterres amefananisha rushwa na shambulizi la kimaadili duniani.

“Hupora  wanajamii haki  yao ya kuwa na shuIe, hospitali na huduma nyingine muhimu, hupoteza uwekezaji wa kigeni na kupora mataifa rasilimali zao za kiasili,” amesema Bwana Guterres.

Halikadhalika amesema rushwa inadidimiza utawala wa kisheria na kusaidia kusongesha uhalifu kama vile usafirishaji haramu wa binadamu, madawa ya kulevya na silaha.

Bwana Guterres ametaja pia ukwepaji kodi na utakasishaji wa fedha kuwa vitendo vinavyochagizwa na rushwa na hivyo kukwamisha maendeleo endelevu.

Tangazo nje ya hospitali katika mji mkuu Monrovia,Liberia, ikiwahimiza wagonjwa wasiwapatie fedha madaktari kama malipo ya huduma yoyote.
UNICEF/Pirozzi
Tangazo nje ya hospitali katika mji mkuu Monrovia,Liberia, ikiwahimiza wagonjwa wasiwapatie fedha madaktari kama malipo ya huduma yoyote.

Amenukuu Benki ya Dunia ambayo inasema kuwa sekta ya biashara na watu binafsi hulipa zaidi ya dola trilioni 1 kila mwaka kama rushwa akisema, “rushwa inasababisha rushwa kuongezeka na kuchochea tabia ya ukwepaji sheria.

Hata hivyo amesema mkataba wa kimataifa dhidi ya rushwa ni mbinu mahsusi na ya msingi ya kutokomeza rushwa.

“Lengo namba 16 la malengo ya maendeleo endelevu pamoja na malengo yake madogo yanatoa mwelekeo wa hatua za kuchukua,” amesema Bwana Guterres akiongeza kuwa kwa kupitia “mfumo wa kujitathmini uliowekwa na mkataba huu, tunaweza kushirikiana kujenga msingi wa kuaminiana na uwajibikaji. Tunaweza kuelimisha  na kujengea uwezo raia, na kusongesha uwazi na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kurejesha mali zilizoporwa.”

Amesema mamilioni ya watu mwaka huu duniani kote walipiga kura huku hoja ya rushw aikiwa ndio kipaumbele kikuu hivyo basi “katika siku ya kimataifa ya kutokomeza rushwa hebu na tusimamie maadili.”

Nayo ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupambamba na madawa ya kulevya na uhalifu, UNODC imeeleza bayana kuwa rushwa inadidimiza taasisi za kidemokrasia, inazororesha maendeleo ya kiuchumi na kukosesha utulivu wa serikali.

Kwa mantiki hiyo ofisi hiyo  imetaka kila mtu achukue hatua kukomesha kitisho hicho.
TAGS: Rushwa, SDGs, Antonio Guterres, UNODC