Vita dhidi ya ufisadi ni chachu kwa SDGs

23 Mei 2018

Rushwa ni adui wa haki, ni kauli ambayo hii leo imepatiwa mkazo wakati wa maadhimisho ya miaka 15 ya mkataba wa kimataifa wa kupambana na rushwa duniani.

Viongozi waandamizi wa Umoja wa Mataifa wamepazia sauti kauli hiyo wakati wa mjadala wa Baraza Kuu la umoja huo jijini New York, Marekani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, katika hotuba yake amesisitiza ubaya wa ufisadi akisema kuwa lengo namba 16 la malengo ya maendeleo endelevu,SDGs, linataka kupunguza ufisadi na rushwa, kuimarisha hatua za kurejesha mali zilizoporwa na kukuza taasisi zilizo wazi.

Bwana Guterres amesema, hakuna taifa kubwa wala dogo linalosalimika na rushwa "na wanaoathirika zaidi na ufisadi ni wale ambao hawatoi rushwa.”

 ufisadi unaathiri mataifa yaliyoendelea na yale yanayoibuka kiuchumi 

Katibu Mkuu amesema matokeo yake kwenye mazingira ya ufisadi, jamii haiwezi kuendelea sawa endapo maafisa husika kuanzia madaktari hadi polisi, majaji na wanasiasa wote wanajitajirisha badala ya kufanya kazi zao kwa heshima.

Kwa upande wake, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Miroslav Lajcak, alisogeza mbele mada ya mkutano kwa kupendekeza  suala la usawa wa jinsia katika  mjadala wa vita dhidi ya ufisadi kwa kuwataka washiriki wa mkutano huo kutosahau kuwahusisha wanawake na wasichana  katika juhudi zote  za kufanikisha SDGs.

Tangazo nje ya hospitali katika mji mkuu Monrovia,Liberia, ikiwahimiza wagonjwa wasitoe hela kwa madaktari kwa huduma yoyote.
UNICEF/Pirozzi
Tangazo nje ya hospitali katika mji mkuu Monrovia,Liberia, ikiwahimiza wagonjwa wasitoe hela kwa madaktari kwa huduma yoyote.

Mkurugenzi Mtendaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayopambana na madawa ya kulevya na uhalifu, UNODC, Yuri Fedotov, amesema, “ili kukuza maendeleo endelevu ni lazima tushirikiane sote kuimarisha juhudi za amani, usalama na kulinda haki za binadamu na ndipo vita dhidi ya ufisadi itashika kasi.”

Kwa mantiki hiyo ametoa wito kwa jumuiya ya kimatifa kusaidia kufanikisha SDGs kwa kutoa takwimu sahihi za kupambana na rushwa.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter