Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ambao hamjaridhia mkataba wa watu wenye ulemavu fanye hima- Guterres

Kuwa na ulemavu siyo ukomo wa maisha.
NICEF/Sebastian Rich
Kuwa na ulemavu siyo ukomo wa maisha.

Ambao hamjaridhia mkataba wa watu wenye ulemavu fanye hima- Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Leo ni siku ya watu wenye ulemavu ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa ujumbe wake akisema kuwa, “tunapolinda haki za watu wenye ulemavu, tunasonga mbele kufikia ahadi kuu ya Ajenda ya 2030 - kutowaacha yeyote nyuma,”  akisema kuwa, hata hivyo bado kuna mengi ya kufanya, tumeona maendeleo muhimu katika kujenga ulimwengu jumuishi kwa wote.

Katibu Mkuu amesema takribani nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa zimeridhia Mkataba wa Haki za watu wenye Ulemavu na hivyo anawahimiza wale ambao bado hawajafanya hivyo kuuridhia bila kuchelewa.

Amekumbusha kuwa, “mnamo mwezi Juni, nilizindua Mkakati jumuishi wa wenye ulemavu wa Umoja wa Mataifa, ili kuinua viwango na utendaji kuhusu ujumuishaji wa watu wenye ulemavu, katika maeneo yote ya kazi yetu na ulimwenguni kote.Na kwa mara ya kwanza, Baraza la Usalama lilipitisha azimio lake la kwanza mahsusi kwa ajili ya ulinzi wa watu wenye ulemavu katika mizozo ya silaha.

Amesisitiza kuwa, Umoja wa Mataifa umeazimia kuongoza kwa mfano na kwa mantiki hiyo, “katika Siku hii ya Kimataifa, ninathibitisha tena azma ya Umoja wa Mataifa kufanya kazi na watu wenye ulemavu kujenga mustakabali endelevu, jumuishi na mustakabali wenye mabadiliko ambao kila mtu, wakiwemo wanawake, wanaume, wasichana na wavulana wenye ulemavu, wanaweza kufikia uwezo wao.”