Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wafanyakazi wa kujitolea India wamewezesha majengo kutumiwa pia na watu wenye ulemavu

Mfanyakazi wa kujitolea katika shirika la msalaba mwekundu nchini Uganda akielimish watu kuhusu hatari za Ebola kupitia bango lililoandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF. Mafunzo hayo kwa watu wanaovuka mpaka kutoka DRC.
UNICEF/Adriko
Mfanyakazi wa kujitolea katika shirika la msalaba mwekundu nchini Uganda akielimish watu kuhusu hatari za Ebola kupitia bango lililoandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF. Mafunzo hayo kwa watu wanaovuka mpaka kutoka DRC.

Wafanyakazi wa kujitolea India wamewezesha majengo kutumiwa pia na watu wenye ulemavu

Masuala ya UM

Leo tarehe 5 Desemba ni siku ya wafanyakazi wa kujitolea duniani ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres anakumbusha kuwa kujitolea ni mfumo thabiti wa kushirikisha jamii hususan ile iliyoachwa nyuma zaidi katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu, SDGs.

Katika ujumbe wake wa siku ya leo yenye maudhui, kujitolea kwa ajili ya mustakabali jumuishi, Bwana Guterres anasema kuwa maudhui hayo ni muhimu kwa kuzingatia kuwa ajenda ya 2030 inataka dunia ambamo kwayo kuna usawa, haki, stahamala na ya uwazi ambako mahitaij ya hata wale walio hatarini zaidi yanatimizwa.

“Wakati watu wanajitolea, wanaungana na wengine na kuimarisha ile hisia ya kuwa na lengo la uwepo wao duniani. Maudhui ya mwaka huu kujitolea kwa mustakabali jumuishi, yanaadhimisha ya kwamba kupitia kujitolea, watu wanakuwa na mchango wenye maana na hivyo kujenga jamii jumuishi na yenye usawa,” amesema Bwana Guterres.

Katibu Mkuu anasema kupitia kujitolewa, watu walio pembezeoni wanakuwa wanajumuishwa zaidi kwenye jamii.

Ametolea mfano wa mpango wa #HerStory au Simulizi yake yenye wahariri wa kujitolea 500 kutoka nchi za kiarabu, imeongeza uwakilishi wa wanawake wanaozungumza lugha ya kiarabu katika kamusi ya maarifa ya mtandaoni, Wikipedia.

“Hatua hii imefanikisha usawa wa kijinsia na ujumuishi katika ukanda huo,”  amesema Katibu Mkuu huku akiongeza kuwa wafanyakazi wa kujitolea wa Umoja wa Mataifa kupitia kampeni ya kuhakikisha watu wote wanaweza kutumia majengo nchini India, wameweza kukagua majengo 1,600 ya umma katika miji 25 na kuwezesha kurahisisha matumizi yake kwa watu wenye ulemavu.

Amesema na katika kambi za wakimbizi duniani kote, wakimbizi wa ndani sasa wanajitolea kusaidia elimu ya watoto na kuimarisha utangamano wa kitamaduni.

Katibu Mkuu anasema pamoja na kuunga mkono shughuli za wafanyakazi wa kujitolea wa Umoja wa Mataifa na kuchagiza kuongezeka kwao ili kufanikisha ajenda 2030, “hebu na tuunge mkono harakati za kujitolea duniani kote kwa kuwa zinakuza mshikamano na maelewano.”

Amekumbusha kuwa kujitolea ni muhimu  katika kuhakikisha malengo ya maendeleo endelevu yanamilikiwa na yanatekelezwa na wananchi wenyewe kwa ajili ya watu wote.

Kwa mantiki hiyo amesema, “katika siku hii ya kimataifa ya wafanyakazi wa kujitolea hebu na tuwashukuru wafanyakazi hao duniani kote amako wanafanya dunia hii iwe jumuishi zaidi na yenye stahamala zaidi.”