Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Teknolojia: Mtazamo wa Maendeleo Jumuishi ya Ulemavu

IOM imesambaza magongo na viti vya magurudumu kwa watu wenye ulemavu.
IOM/Monica Chiriac
IOM imesambaza magongo na viti vya magurudumu kwa watu wenye ulemavu.

Teknolojia: Mtazamo wa Maendeleo Jumuishi ya Ulemavu

Haki za binadamu

Leo ni siku ya Kimataifa ya watu wenye ulemavu, maadhimisho ya siku hii yanafanyika kwa njia ya mtandao yakibeba maudhui yasemayo “Kupunguza Kutokuwepo kwa Usawa Kupitia Teknolojia: Mtazamo wa Maendeleo Jumuishi ya Ulemavu,” 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wa maadhimisho ya siku hii ameeleza kuwa Covid-19 imeweka wazi vikwazo vinavyoendelea na ukosefu wa usawa unaokabiliwa na watu bilioni 1 wenye ulemavu duniani, ambao wamekuwa miongoni mwa walioathirika zaidi na janga hilo.

“Hatua ya kushughulikia janga inayojumuisha ulemavu inapaswa kuongozwa na watu wenye ulemavu wenyewe, kuunda ubia, kukabiliana na ukosefu wa haki na ubaguzi, kupanua ufikiaji wa teknolojia na kuimarisha taasisi ili kuunda ulimwengu unaojumuisha zaidi, inayofikika na endelevu baada ya COVID-19.” Ameshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Guterres. 

Hakuna chochote kutuhusu bila sisi 

Aidha Guterres amehimiza nchi zote duniani kutekeleza kikamilifu mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu, akisema hii itasaidia kuongeza ufikiaji, na kuondoa vikwazo vya kisheria, kijamii, kiuchumi na vingine vyovvyote  kwa ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu na mashirika yanayo wawakilisha. 

"Kutambua haki, uharaka, na uongozi wa watu wenye ulemavu kutaendeleza mustakabali wetu wa pamoja. Tunahitaji kila mtu, ikiwa ni pamoja na watu wenye ulemavu kwenye bodi ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs. Ulimwenguni kote, watu wenye ulemavu na mashirika yanayowawakilisha wanachukua hatua kutimiza wito huu: ‘Hakuna chochote kutuhusu, bila sisi’.” Anasisitiza Bwana Guterres.

Mvulana mlemavu anaendelea na masomo wakati wa janga la COVID-19 huko Armenia.
© UNICEF/Grigoryan
Mvulana mlemavu anaendelea na masomo wakati wa janga la COVID-19 huko Armenia.

Yote inamaanisha yote 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni UNESCO, Audrey Azoulay kupitia ujumbe wake wa siku hii amesema janga la ugonjwa wa virusi vya corona linaendelea kuathiri vibaya watu wenye ulemavu na “ni miongoni mwa waathirika wa kwanza wa janga la kiuchumi linalosababishwa na janga hili la Covid-19. Ukosefu wa usawa wa kijamii unachangiwa na ukosefu wa usawa katika ufikiaji wa taarifa, kwa sababu ya ukosefu wa upatikanaji wa mwongozo wa afya katika Nukta nundu au Braille au lugha ya ishara ni ukumbusho wa haja ya kuchukua hatua ili kuhakikisha kuwa taarifa inapatikana kwa kila mtu.”

Bi Azoulay amesema kama sehemu ya maisha yetu yameendamtandaoni, hatua za kufungiwa zimeweka mbele mfululizo mwingine wa ukosefu wa usawa unaoathiri watu wenye ulemavu: ukosefu wa usawa unaohusiana na teknolojia na ulimwengu wa kidijitali.

“Katika uhusiano huo, katika kikao chake cha hivi karibuni zaidi, Mkutano Mkuu wa UNESCO ulipitisha waraka muhimu: Pendekezo la Maadili ya Akili Bandia. Mafanikio haya makubwa ndiyo chombo cha kwanza cha kuweka viwango vya kimataifa katika kikoa hiki. Inalenga kuhakikisha kuwa ukosefu wa usawa na ubaguzi uliopo katika ulimwengu wa kweli hauimarishwi katika ulimwengu wa mtandaoni.” Anaeleza Mkuu huyo wa UNESCO kuhusu hatua Madhubuti wanazozichukua.

Kisha Azoulay anaweka ahadi akisema UNESCO itaendelea kufanya kazi bila kuchoka ili kuona kuwa kuna usawa zaidi katika nyanja ya elimu pia. “Kwa kuzingatia mamlaka yetu, tumejitolea kuunga mkono elimu-jumuishi kwa sababu, kwa kunukuu Ripoti ya Ufuatiliaji wa Elimu Duniani (GEM) ya mwaka 2020, "yote inamaanisha yote". Ripoti ya GEM inabainisha kwamba wakati asilimia 68 ya nchi zina ufafanuzi wa elimu-jumuishi, ni asilimia 57 tu ndio hutaja makundi yote yaliyotengwa.”